Tuesday, July 26, 2016

IRINGA KUWAENZI MASHUJAA KWA KUFANYA KAZI



  Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wakazi wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kuwaenzi mashujaa waliopigana vita vya ukombozi kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa lengo la kujiondolea umasikini na kujiletea maendeleo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akitoa salamu za Mkoa katika maadhimisho ya siku ya mashujaa katika mkoa wa Iringa iliyofanyika katika uwanja wa mashujaa Manispaa ya Iringa.
Masenza alisema “leo tunaenzi kumbukumbu ya mashujaa wa nchi yetu, ambao walipigana vita kutetea uhuru na heshima ya nchi yetu na ulinzi wa mipaka yetu. Katika kuwaenzi mashujaa wetu wananchi wanatakiwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kujiondolea umasikini”. Aliongeza kuwa mashujaa wa nchi hii walipigania ukombozi wa nchi kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

Masenza ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka wananchi kudumisha umoja na mshikamano mkoani hapa akielezea kuwa umoja na mshikamano ndiyo nyenzo ya kuwaletea maendeleo wananchi. Aliwataka wananchi kupinga matendo yanayolenga kuhatarisha amani na usalama wa nchi. Aliongeza kuwa usalama wa mkoa pamoja na mambo mengine, unategenea pia malezi sahihi ya watoto. 

Aidha, aliwataka wazazi na jamii kwa ujumla kuwalea watoto katika misingi inayokubalika ili wawe raia wema na wazalendo kwa nchi yao. Alisema kuwa uzalendo wa kweli unategemea sana na malezi sahihi ya watoto. 

Nae Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa hali ya usalama katika Wilaya ya Iringa ni shwari kutokana na vyombo vya ulinzi kuwa vimejipanga vizuri. “Wilaya ya Iringa tunaweza kulala usingizi vizuri kwa sababu wapo watu wanaokesha kwa ajili ya usingizi wetu na watu hao ni vyombo vya usalama” alisema Kasesela. Aidha, aliwasilisha ombi kwa Meya wa Manispaa ya Iringa kutenga eneo lingine la kuadhimishia maadhimisho ya mashujaa kubwa ambalo litatoa wigo kwa wananchi wengi zaidi kushuhudia maadhimisho hayo tofauti na eneo la sasa.
=30=

WATUMISHI SERIKALI ZA MITAA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WAKURUGENZI WAPYA IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa watakiwa kutoa ushirikiano mzuri Wakurugenzi walioteuliwa hivi karibuni na Rais ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alioikuwa akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini Iringa jana.


Jafo alisema kuwa ili Wakurugenzi waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ushirikiano baina ya watumishi na wakuu wa idara ni muhimu na kuwataka watumishi hao kuwapa ushirikiano mzuri Wakurugenzi hao wateule. “Wakurugenzi wapya hakikisheni mnatengeneza mtandao mzuri na wafanyakazi wote. Wapo baadhi ya watumishi kazi yao ni kutengeneza makundi ya fitna kwa Wakurugenzi ili wawachukie baadhi ya watumishi. Mkurugenzi ukikumbatia watumishi wa aina hiyo, basi watumishi hao watakupeleka mahali pabaya” aliongeza Jafo.


Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Naibu Waziri alisema kuwa haridhishwi na ukusanyaji mapato hasa vijijini ambapo maeneo mengi hayatumii mfumo wa kieletroniki katika kukusanya mapato ya serikali. “Mapato ya ndani yanaathiriwa sana na mfumo dhaifu wa ukusanyaji mapato, ndiyo maana maelekezo ya serikali ni kutumia mfumo wa kieletroniki katika kukusanya mapato. Mapato ya ndani yasipokusanywa yanatuathiri sote na kushindwa kutekeleza majukumu yetu ikiwa ni pamoja na kwenda vijijini kwa wananchi kufanya kazi” aliongeza Jafo.

Alisema kuwa wapo baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao wametengeneza mfumo wa ulaji kupitia mfumo wa ukusanyaji mapato ya Halmashauri na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwa makini katika kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ya serikali.

Naibu Waziri huyo, alisema “agenda ya Rais, John Magufuli ni mabadiliko ya kiuchumi, na wananchi wote wanataka mabadiliko ya kweli. Mabadiliko hayo lazima yaletwe na watumishi wa Halmashauri kwa kutimiza wajibu wao katika kufanya kazi. Kama sekta ya maji, afya, elimu, ujenzi na sekta nyingine hazitaenda sawa katika kutekeleza majukumu yake ni dhahiri kuwa wananchi watailalamikia serikali yao, malalamiko hayo yatatokana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri kutotimiza wajibu wao”.

Alimshauri Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kupitia taarifa za kibenki za Halmashauri hiyo na kujiridhisha na mwenendo wa matumizi ya fedha za serikali kabla ya kuingia katika vikao vya Kamati ya fedha ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha za serikali.
=30=