Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watumishi
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa watakiwa kutoa ushirikiano mzuri Wakurugenzi walioteuliwa
hivi karibuni na Rais ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kauli
hiyo ilitolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Selemani Jafo alioikuwa akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Iringa katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini Iringa jana.
Jafo
alisema kuwa ili Wakurugenzi waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,
ushirikiano baina ya watumishi na wakuu wa idara ni muhimu na kuwataka watumishi
hao kuwapa ushirikiano mzuri Wakurugenzi hao wateule. “Wakurugenzi wapya hakikisheni mnatengeneza mtandao mzuri na wafanyakazi
wote. Wapo baadhi ya watumishi kazi yao ni kutengeneza makundi ya fitna kwa Wakurugenzi
ili wawachukie baadhi ya watumishi. Mkurugenzi ukikumbatia watumishi wa aina
hiyo, basi watumishi hao watakupeleka mahali pabaya” aliongeza Jafo.
Kuhusu
ukusanyaji wa mapato, Naibu Waziri alisema kuwa haridhishwi na ukusanyaji
mapato hasa vijijini ambapo maeneo mengi hayatumii mfumo wa kieletroniki katika
kukusanya mapato ya serikali. “Mapato ya
ndani yanaathiriwa sana na mfumo dhaifu wa ukusanyaji mapato, ndiyo maana
maelekezo ya serikali ni kutumia mfumo wa kieletroniki katika kukusanya mapato.
Mapato ya ndani yasipokusanywa yanatuathiri sote na kushindwa kutekeleza
majukumu yetu ikiwa ni pamoja na kwenda vijijini kwa wananchi kufanya kazi”
aliongeza Jafo.
Alisema
kuwa wapo baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao wametengeneza mfumo wa
ulaji kupitia mfumo wa ukusanyaji mapato ya Halmashauri na kumtaka Mkurugenzi
wa Halmashauri hiyo kuwa makini katika kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ya
serikali.
Naibu
Waziri huyo, alisema “agenda ya Rais,
John Magufuli ni mabadiliko ya kiuchumi, na wananchi wote wanataka mabadiliko
ya kweli. Mabadiliko hayo lazima yaletwe na watumishi wa Halmashauri kwa
kutimiza wajibu wao katika kufanya kazi. Kama sekta ya maji, afya, elimu,
ujenzi na sekta nyingine hazitaenda sawa katika kutekeleza majukumu yake ni
dhahiri kuwa wananchi watailalamikia serikali yao, malalamiko hayo yatatokana
na baadhi ya watumishi wa Halmashauri kutotimiza wajibu wao”.
Alimshauri
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kupitia taarifa za kibenki za Halmashauri hiyo na
kujiridhisha na mwenendo wa matumizi ya fedha za serikali kabla ya kuingia
katika vikao vya Kamati ya fedha ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha
za serikali.
=30=
No comments:
Post a Comment