Tuesday, March 5, 2013

SERIKALI YATETA NA RC


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Mahusiano na Uhusiano, Stephen Wassira akiongea na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania, Askofu Tarcisius  Ngalalekumtwa alipotembelea makazi ya Askofu huyo mjini Iringa. Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

BARAZA LA BIASHARA LA MKOA LIKABILI CHANGAMOTO



IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wajumbe wa Baraza la biashara la Mkoa kuzikabili changamoto mbalimbali zinazokabili utendaji kazi wa baraza hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akifungua mkutano wa maandalizi ya baraza la biashara la 
Mkoa wa Iringa katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa baraza la biashara linazo changamoto lukuki katika utekelezaji wa majukumu yake. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa wajumbe walio na dhamira na wakilishi wa dhati katika baraza. Amesema upatikanaji wa fedha za kuendesha vikao, tafiti na ufuatiliaji pia ni changamoto.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameyataja madhumuni na kazi za baraza la Mkoa kuwa ni pamoja na kutoa utaratibu kwa ajili ya madiliano na mazungumzo ya Sekta ya Umma na binafsi kwa lengo la kufikia muafaka kuhusu masuala ya kimkakati yanayohusiana na usimamizi thabiti wa rasilimali za maendeleo.

Amesema majukumu mengine ni kubadilishana mawazo kuhusu mazingira ya uendeshaji na taratibu za pamoja na kupendekeza njia za kurahisisha huduma za umma, kuboresha utoaji wa huduma za umma, kuongeza mahusiano mazuri na sekta binafsi. Mengine ni kupitia kila mara maendeleo katika mazingira ya biashara ya ndani na nje, changamoto na fursa zinazoletwa Iringa na kujadili hatua za kuchukua.

Dkt. Christine ameyataja madhumuni mengine kuwa ni kupitia upya na kupendekeza mabadiliko katika mazingira ya Sera mbalimbali ili kuongeza uvutiaji wa vitega uchumi vya ndani na nje, na kuboresha ushindani wa bidhaa bora za Tanzania katika soko la nje. Amesema kuhimiza na kukuza uanzishwaji  wa Sera na utaratibu wa masuala ya kijamii na kiuchumi.

Ikumbukwe kuwa mabaraza ya biashara yalianzishwa kwa waraka wa Rais, Namba 1 wa mwaka 2001 kwa lengo la kukuza na kuendeleza majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi nchini.
=30=

SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA WADAU WA SEKTA YA AFYA



IRINGA

Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa na kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini kwa lengo la kumuhudumia vizuri mwananchi.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba wakati wa ufunguzi wa jengo la huduma ya upasuaji wa macho pamoja na kituo cha huduma ya kupima na kutengeneza miwani katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa sababu Serikali peke yake haiwezi kutekeleza jukumu hilo.

Akiongelea ufunguzi wa jengo la huduma ya upasuaji wa macho pamoja na kituo cha huduma ya kupima na kutengeneza miwani, amesema kuwa shughuli hiyo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 70 zikiwa ni ukarabati wa jengo la huduma ya upasuaji. Amesema shilingi milioni 35 zimetumika kununua vifaa tiba vilivyopo katika kituo cha kupima na kutengeneza miwani zikiwa ni misaada kutoka mashirika ya Sightsavers na taasisi ya Brien Holden Vision.

Amesema kuwa mashirika hayo yameonesha dhamira ya wazi ya kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza Sera ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za jamii.

Aidha, amewataka watumishi wa idara ya afya hasa huduma za macho kuhakikisha wanatumia msaada huo kwa malengo yaliyokusudiwa. Kwa wasimamizi wa huduma za afya katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kuhakikisha vifaa vyote vilivyotolewa na wadau vinaingizwa katika leja ya hospitali na kutunzwa kwa kufanyiwa matengenezo na matengeneza kinga kama inavyotakiwa ili viweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Katika taarifa ya huduma za mradi jumuishi wa macho Iringa iliyowasilishwa na Daktari bingwa wa macho katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa, Dkt. George Kabona amesema kuwa shughuli za mradi jumuishi wa huduma za macho mkoani Iringa ulianzishwa mwaka 1998 kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers. 

Amesema kuwa lengo kubwa la mradi huo ni kuhakikisha watu wote wenye upofu unaozuilika wanapatiwa huduma ya kuepukana na upofu huo na wale wenye upofu usiozuilika wanapatiwa elimu bora hasa watoto.

Dkt. Kabona amezitaja shughuli za mradi huo zilizogawanyika katika sekta tatu kuwa ni afya ya macho, elimu jumuishi na utengamao.

Akiongelea mafanikio ya mradi huo, amesema kuwa sekta hiyo imepata mafanikio makubwa na kuyataja kuwa ni pamoja na kuweza kuwaona na kuwapatia huduma wagonjwa 76,471 katika mkoa mzima wa Iringa kati ya mwaka 2009-2011. Mafanikio mengine ni kufanyika kwa upasuaji kwa wagonjwa 6,280 katika kipindi hicho.

=30=



=30=