Tuesday, March 5, 2013

BARAZA LA BIASHARA LA MKOA LIKABILI CHANGAMOTO



IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wajumbe wa Baraza la biashara la Mkoa kuzikabili changamoto mbalimbali zinazokabili utendaji kazi wa baraza hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akifungua mkutano wa maandalizi ya baraza la biashara la 
Mkoa wa Iringa katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa baraza la biashara linazo changamoto lukuki katika utekelezaji wa majukumu yake. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa wajumbe walio na dhamira na wakilishi wa dhati katika baraza. Amesema upatikanaji wa fedha za kuendesha vikao, tafiti na ufuatiliaji pia ni changamoto.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameyataja madhumuni na kazi za baraza la Mkoa kuwa ni pamoja na kutoa utaratibu kwa ajili ya madiliano na mazungumzo ya Sekta ya Umma na binafsi kwa lengo la kufikia muafaka kuhusu masuala ya kimkakati yanayohusiana na usimamizi thabiti wa rasilimali za maendeleo.

Amesema majukumu mengine ni kubadilishana mawazo kuhusu mazingira ya uendeshaji na taratibu za pamoja na kupendekeza njia za kurahisisha huduma za umma, kuboresha utoaji wa huduma za umma, kuongeza mahusiano mazuri na sekta binafsi. Mengine ni kupitia kila mara maendeleo katika mazingira ya biashara ya ndani na nje, changamoto na fursa zinazoletwa Iringa na kujadili hatua za kuchukua.

Dkt. Christine ameyataja madhumuni mengine kuwa ni kupitia upya na kupendekeza mabadiliko katika mazingira ya Sera mbalimbali ili kuongeza uvutiaji wa vitega uchumi vya ndani na nje, na kuboresha ushindani wa bidhaa bora za Tanzania katika soko la nje. Amesema kuhimiza na kukuza uanzishwaji  wa Sera na utaratibu wa masuala ya kijamii na kiuchumi.

Ikumbukwe kuwa mabaraza ya biashara yalianzishwa kwa waraka wa Rais, Namba 1 wa mwaka 2001 kwa lengo la kukuza na kuendeleza majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi nchini.
=30=

No comments:

Post a Comment