Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa
wa Iringa wametakiwa kusimamia vizuri miradi na fedha za Serikali ili kudhibiti
matumizi mabaya na hoja zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokusimamia vizuri
fedha na miradi hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma, wakati akifungua
kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo katika
Wilaya ya Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa katika
agenda zitakazojadiliwa ni utekelezaji wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali. “Ninalowasihi ndugu wajumbe, kwa mwaka huu, kuanzia sasa
ni kusimamia miradi na fedha ambazo Halmashauri hupewa na Serikali, ili
kudhibiti ubadhilifu wa fedha na hoja zinazoweza kujitokeza” asilisitiza Dkt.
Christine. Aidha, aliwashauri kutokuanzisha miradi mipya wakati miradi ya
zamani haijakamilika na kuwataka kumaliza miradi viporo kwanza ndipo waanzishe
miradi mipya.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, aliwashauri wajumbe wa kikao hicho kuwashauri wakulima
wanaoishi katika maeneo yenye upungufu wa mvua, kulima mazao yanayovumilia
ukame. Amesema “nichukue fursa hii kuwaomba kufikisha ujumbe kwa wakulima
wanaoishi maeneo yenye upungufu wa mvua, kuwa ni vizuri wakulima walime mazao
ya mtama na alizeti ambayo yanavumilia ukame”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa alitumia kikao
hicho kuwataka wajumbe kusimamia suala la utunzaji wa mazingira ambayo kwa sasa
yanaharibiwa kwa kasi kubwa na shughuli za binadamu.
Wakati huo huo, Sekretarieti ya Mkoa
wa Iringa imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi 950,000,000 kwa mwaka wa
fedha 2011/ 2012.
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji
wa Mpango na bajeti kwa kipindi cha Julai-Juni, 2011/ 2012, Katibu Tawala
Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Nuhu Mwasumilwe amesema kuwa kwa mwaka
wa fedha 2011/2012, Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa ilikadiriwa kukusanya jumla
ya shilingi 903,000. Amesema hadi kufikia mwezi Juni, 2012 jumla ya shilingi
950,895,762 zimekusanywa kwa mchanganuo ufuatao, marejesho ya mishahara ni shilingi
949,591,700, kodi ya pango la nyumba ni shilingi 636,238 na ada ya ufuatiliaji
shilingi 19,000.
Mwasumilwe amesema kwa upande wa
Serikali za Mitaa, katika kipindi cha mwaka 2011/ 2012, Halmashauri za Wilaya,
Miji na Manispaa zilitarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 8,342,138,599 kutoka
katika vyanzo vyake vya mapato vya ndani. Amesema hadi kufikia mwezi Juni, 2012
jumla ya shilingi 7,358,634,981 zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 88.2 ya
lengo.