Monday, September 3, 2012

VIJIJI VIFUTWE MANISPAA YA IRINGA



Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imekuwa ikishindwa kutekeleza baadhi ya mikakati ya mipango ya mji na mipango mingine ya maendeleo kutokana na uwepo wa vijiji saba, jambo linaloleta mkanganyiko wa kiutendaji ndani ya Manispaa.

Akiwasilisha mapendekezo ya kufuta vijiji katika Manispaa ya Iringa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Theresia Mahongo ameitaja sababu kuu ya Halmashauri kutaka kufutwa kwa vijiji hivyo kuwa ni Halmashauri ya Manispaa kupanua mipaka yake kama inavyoelekezwa kwenye fungu la 12 la ‘The Local Government (Urban Authorities) Act, 1982. Amesema kifungu cha 12 kijifungu (1) kinasema kwamba Waziri mwenye dhamana anaweza kutangaza kwenye Gazeti la Serikali kufuta kijiji ama kijiji cha ujamaa kilichoingia kwenye mipaka ya eneo la Mji. 

Akielezea hali halisi, Theresia amesema kuwa Manispaa yake imekuwa ikipata matatizo ya kiutendaji katika maeneo ya vijiji husika na kusababisha baadhi ya mikakati ya mipango ya mji na mipango mingine kutokukamilika. Ameyataja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni kufanana kwa baadhi ya kazi za Halmashauri ya Manispaa na Halmashauri ya kijiji jambo linalosababisha kupingana katika suala la kiutendaji na utoaji wa maamuzi. Vilevile, amesema mvutano katika kutekeleza mipango thabiti na madhubuti ya Halmashauri ya Manispaa katika eneo lake la kiutawala na kusababisha baadhi ya mipango kutokutekelezwa katika maeneo ya kiutawala ya kijiji.

Matatizo mengine Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa ameyataja kuwa ni suala la Ardhi ambalo limekuwa ni kikwazo kikubwa katika Mpango wa Mji na vijiji, kwa kuzingatia Sheria zinazolinda vijiji, vijiji vimepewa ruhusa ya kuuza, kuzuia na kuendeleza Ardhi ya kijiji bila ya kuingiliwa na mamlaka yoyote. Ameongeza kuwa Sheria ya Ardhi ya vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 8(1) kinaeleza kuwa Halmashauri ya kijiji kwa kuzingatia masharti ya Sheria hii itawajibika kusimamia Ardhi yote ya kijiji. Amesema kwa tafsiri ya kifungu hicho, Halmashauri ya Manispaa ambayo ndiyo inayoshughulika na Mpango wa Mji, haitakuwa na mamlaka kuingia na kutekeleza Mpango wowote wa Mji katika eneo la kijiji.

Theresia ameyataja manufaa yatakayopatikana baada ya kufutwa vijiji kuwa ni pamoja na Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi inayojumuisha huduma muhimu na za msingi kwa jamii inayozingatia Sheria, pamoja na kuongezeka kwa thamani ya Ardhi kutokana na maeneo kupimwa na kupata hati milki. Ongezeko la hali ya kiuchumi na kipato kwa jamii kutokana na kutumia hati katika kuomba mikopo katika asasi za kifedha. Manufaa mengine ameyataja kuwa ni kupungua na kuisha kabisa kwa migogoro na migongano ya Ardhi isiyokuwa ya lazima kutokana na kuzingatia Sheria na Mipango iliyowekwa.

Akitoa hoja, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa amesema ili kukabiliana na changamoto za kiutawala na kiutendaji, ni muafaka hatua madhubuti zichukuliwe kufuta vijiji vyote ndani ya eneo la Halmashauri ya Manispaa ili kurahisisha utendaji na utekelezaji wa mipango endelevu katika maeneo yanayomilikiwa na vijiji kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa inavyo vijiji saba vilivyosajiliwa kisheria, ambavyo ni Igumbilo, Kigonzile, mgongo, Nduli, Itamba, Mkoga na Kitwiru.

No comments:

Post a Comment