Wauguzi Mkoani Iringa wametakiwa
kutumia mafunzo waliyopata ya kuwajengea uwezo katika kutoa huduma nzuri kwa
kuzingatia miiko na maadili ya kazi zao ili mwananchi aweze kunufaika na huduma
zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Robert Salim alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili
ya kuwajengea uwezo katika utoaji huduma Wauguzi kutoka katika taasisi za
serikali na binafsi Mkoani hapa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dr. Robert Salim akifunga mafunzo ya Wauguzi
Dkt. Salim amesema “tumieni mafunzo
mliyoyapata katika kuboresha huduma za afya katika mkoa wetu wa Iringa”.
Amewaasa wauguzi hao kuwa wanao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma
kwa kufuata miiko na maadili ya taaluma zao katika kuihudumia jamii. Amesema
lengo la ushirika baina ya serikali na sekta binafsi ni kuhakikisha mwananchi
anapata huduma bora kwa upande mmoja na mtoa huduma kuendelea kutoa huduma
katika mazingira salama. Amesema kuwa mafunzo hayo pia yamelenga maeneo yenye
changamoto hatarishi kama kuzuia maambukizi ya maradhi baina ya mtoa huduma na
mpokea huduma, maadili kwa wauguzi na jinsi ya kupambana na kuzuia magongwa ya
kuambukiza.
Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa amewataka
waganga wakuu wa Wilaya kuanza kufikiria kuingiza katika bajeti na mipango ya
maendeleo ya Halmashauri programu za mafunzo ya kuwajengea uwezo wauguzi ili
kuyafanya mafunzo hayo yawe endelevu hata baada ya mradi huo kukamilika
mwishoni mwa mwaka 2013.
Akielezea matarajio baada ya mafunzo
hayo, Mratibu wa mafunzo, Veronica James amesema kuwa matarajio yake ni wauguzi
kutoa huduma kitaalamu na kitaaluma zaidi, na uwezo wa kufikisha huduma bora
kwa wananchi. Amesema lengo la mafunzo hayo kutolewa kwa wauguzi katika mkoa wa
Iringa pia ni kupunguza na hatimae kuondoa kabisa dhana ya huduma zisizo za
kuridhisha kwa baadhi ya wauguzi Mkoani Iringa.
James ambae pia ni Meneja wa
Hospitali ya Agakhan- Iringa amesema kuwa ili huduma ziweze kuwa bora zaidi
dhana ya ushindani lazima ijengeke niongoni mwa wauguzi katika kutoa huduma
bora. Amesema kuwa pamoja na kwamba baadhi ya mambo wauguzi wameyasoka wakiwa
vyuoni lakini ipo haja ya kuendelea kuwakumbusha ili kuwaamsha zaidi katika
kukabiliana na changamoto na utoaji huduma za kila siku.
Akielezea mafanikio ya mradi huo,
Daidu Beyai, Mratibu wa Mradi huo amesema kuwa lengo mahususi la mradi huo ni
kuwajengea uwezo wauguzi ili waweze kutoa huduma bora za afya katika Mkoa wa
Iringa kwa kuwaongezea ulimu na ujuzi. Ameyataja mafanikio makubwa katika
kipindi cha miaka mitatu kuwa ni kuwapatia mafunzo wauguzi 510 katika Mkoa wa
Iringa. Amesema katika kufuatilia utekelezaji na ufanisi wa mafunzo hayo kwa
wauguzi, tathmini imekuwa ikifanyika kabla ya mafunzo na baada ya mafunzo ili
kuona kama mafunzo hayo yanatoa matokeo chanya. Amesema kwa mujibu wa tathmini
hiyo wauguzi waliopatiwa mafunzo hayo wameendelea kufanya vizuri katika
utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuongeza elimu na ujuzi.
Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo,
Eligia Lwela, Muunguzi katika hospitali ya Wilaya ya Mufini, amesema kuwa
mafunzo hayo yamemsaidia kuboresha utoaji wake huduma na kuleta ufanisi mkubwa
wa kazi yake. Aidha, ameomba mafunzo hayo yawe endelevu ili yaweze kuwafikia
wauguzi wote katika Mkoa wa Iringa.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo wauguzi
katika Mkoa wa Iringa yamefadhiliwa na Shirika la misaada la Marekani kupitia
mradi wa Intra Health na kusimamiwa na Hospitali ya Agakhan Iringa.
No comments:
Post a Comment