Vyombo vya habari Mkoani Iringa
vimeshauriwa kuendelea kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili liweze
kufanikiwa katika Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.
Rai
hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi
baada ya kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza usiku wa
Kuamkia leo nchini kote.
Dkt.
Christine amesema kuwa zoezi hilo vimeanza vizuri na mdadisi ameonekana kubobea
katika kazi hiyo. Aidha, amewamwagia sifa wakufunzi na wadadasi kwa jinsi
walivyoonesha juhudi katika kufundisha na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu
uelewa wa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi.
Dr. Christine Gabriel Ishengoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Sensa ya Mkoa
amevipongeza vyombo vya habari vya Mkoa wa Iringa kwa weledi katika kuhamasisha
zoezi hili. Amesema uhamasishaji ni muhimu sana katika kutoa hamasa kwa kazi ya
Sensa ili asitokee mtu ambaye atakuwa hakupata taarifa na elimu juu ya umuhimu
wa Sensa na kuhesabiwa. Aidha, ametoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea na
uhamasishaji huo kwa kipindi cha wiki nzima ili kulifanikisha zoezi hili katika
Mkoa wa Iringa. “kufanikiwa kwa zoezi hili Mkoani Iringa sit u kutakuwa na
manufaa kwa Mkoa wetu, bali kwa nchi nzima na jambo hili litafikiwa pale tu
wananchi wote watakapokuwa wameelewa umuhimu wa zoezi hili na kushiriki katika
kulifanikisha” alisisitiza Dkt. Christine.
Akiongelea
matukio yasiyo ya kawaida katika zoezi hili, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa
wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo limeanza katika hali ya utulivu mkubwa na
hakuna tukio lolote lisilo la kawaida lililotokea na kuripotiwa. Aidha, amewata
wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa pindi watakapopita
katika maeneo yao na kujibu kwa usahihi maswali watakayokuwa wakiulizwa.
Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka, akitoa maoni yake baada ya kuhesabiwa
asubuhi ya leo amesema kuwa kazi ya kuhesabu na kuhesabiwa ni jukumu la kila
mtanzania pasipo kujali mipaka ya aina yoyote. Amesema kila mtanzania anayo
haki ya kuhesabiwa katika Sensa hii ili kuhakikisha Serikali yake inapata
taarifa sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mpaka
amesema “miongoni mwa michango ya wananchi katika jitihada za kujiletea
maendelea kwa kushirikiana na Serikali yao ni pamoja na kushiriki katika Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka huu”. Amesema zipo njia mbalimbali za kushiriki
katika shughuli za maendeleo katika kipindi hiki kutoa taarifa sahihi ni jukumu
namba moja ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi.
Sensa
ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini ikiongozwa na kaulimbiu
isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya
kwanza nchini kote na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi
anahesabiwa mara moja tu.
=30=
No comments:
Post a Comment