Sunday, August 26, 2012

SENSA YAANZA VIZURI MUFINDI



Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Wilayani Mufindi limeanza kwa hali ya utulivu mkubwa na wananchi wameendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Akiongea katika mahojiano maalumu na na gazeti la Uhuru, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amesema kuwa katika siku ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi Wilayani Mufindi, “kwa kweli zoezi hili lilianza saa sita kamili usiku katika maeneo ambayo si ya makazi ya kudumu, kazi ilifanyika katika Mji wa Mafinga katika maeneo ya stendi, nyumba za kulala wageni na maeneo yanapopaki magari makubwa ya mizigo. Aidha, zoezi kama hilo lilifanyika pia katika maeneo ya Nyololo, Igowole, Kibao, Malangali, Ihowanza, Mgololo na Usokami hadi asubuhi saa kumi na moja kazi hiyo ilikuwa imekamilika kwa mafanikio makubwa”. Amesema kuwa leo asubuhi pamoja na kuanza zoezi kwenye makazi ya watu, wagonjwa waliolazwa kwenye vituo vyote vya huduma wamehesabiwa asubuhi na zoezi linaendelea kwenye makazi ya kudumu ya watu.

Akiongelea tathmini yake, amesema kuwa kazi ya kuhesabu watu inaendelea vizuri sana na muitikio wa watu ni mkubwa sana katika zoezi hilo. Amesema ukubwa wa muitikio wa watu katika wilaya yake unatokana uhamasishaji mkubwa unaoendelea kufanyika na kiu kubwa waliyonayo wananchi ya kushirikiana na Serikali katika kujiletea maendeleo.

Evarista ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amesema kuwa ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kwa asilimia 100, viongozi na jamii kwa ujumla hawana budi kuendelea kutoa hamasa na elimu ili wananchi wote waweze kushiriki kikamilifu katika upatikanaji wa takwimu hizo muhimu kwa mustakabali wa taifa. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa wanaoendelea kupita katika kaya zao kukusanya taarifa mbalimbali. Amesema wananchi watakapo jibu kwa usahihi maswali watakayoulizwa na makarani wa Sensa watakuwa wametimiza wajibu wao wa kushiriki katika kupanga mipango ya maendeleo yao kwa namna moja ama nyingine.

Katika mahojiano kwa njia ya simu na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Iringa, Fabian Fundi amesema, “kwa ujumla zoezi hili linaenda vizuri na tulianza saa sita usiku na kuendelea nalo hadi alfajiri. Na asubuhi hii tumeanza kuhesabu kaya binafsi ambazo ni makazi ya kudumu ya watu”. Amesema kuwa kamati ya Sensa Mkoa haijapata taarifa wala matukio yasiyo ya kawaida wala kupokea simu yoyote kutoka kwa makarani kutaarifu kuwa kuna mtu au kaya iliyogoma kuhesabiwa, hii ni dalili nzuri kuwa zoezi hili litakuwa la mafanikio katika Mkoa wa Iringa.

Sensa ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini kote ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo: Jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya kwanza na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa mara moja tu.
=30=

No comments:

Post a Comment