Sunday, August 26, 2012

VYOMBO VYA HABARI IRINGA VYATAKIWA KUENDELEA KUHAMASISHA SENSA



Vyombo vya habari Mkoani Iringa vimeshauriwa kuendelea kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili liweze kufanikiwa katika Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi baada ya kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza usiku wa Kuamkia leo nchini kote.
Dkt. Christine amesema kuwa zoezi hilo vimeanza vizuri na mdadisi ameonekana kubobea katika kazi hiyo. Aidha, amewamwagia sifa wakufunzi na wadadasi kwa jinsi walivyoonesha juhudi katika kufundisha na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uelewa wa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Sensa ya Mkoa amevipongeza vyombo vya habari vya Mkoa wa Iringa kwa weledi katika kuhamasisha zoezi hili. Amesema uhamasishaji ni muhimu sana katika kutoa hamasa kwa kazi ya Sensa ili asitokee mtu ambaye atakuwa hakupata taarifa na elimu juu ya umuhimu wa Sensa na kuhesabiwa. Aidha, ametoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea na uhamasishaji huo kwa kipindi cha wiki nzima ili kulifanikisha zoezi hili katika Mkoa wa Iringa. “kufanikiwa kwa zoezi hili Mkoani Iringa sit u kutakuwa na manufaa kwa Mkoa wetu, bali kwa nchi nzima na jambo hili litafikiwa pale tu wananchi wote watakapokuwa wameelewa umuhimu wa zoezi hili na kushiriki katika kulifanikisha” alisisitiza Dkt. Christine.

Akiongelea matukio yasiyo ya kawaida katika zoezi hili, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo limeanza katika hali ya utulivu mkubwa na hakuna tukio lolote lisilo la kawaida lililotokea na kuripotiwa. Aidha, amewata wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa pindi watakapopita katika maeneo yao na kujibu kwa usahihi maswali watakayokuwa wakiulizwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka, akitoa maoni yake baada ya kuhesabiwa asubuhi ya leo amesema kuwa kazi ya kuhesabu na kuhesabiwa ni jukumu la kila mtanzania pasipo kujali mipaka ya aina yoyote. Amesema kila mtanzania anayo haki ya kuhesabiwa katika Sensa hii ili kuhakikisha Serikali yake inapata taarifa sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mpaka amesema “miongoni mwa michango ya wananchi katika jitihada za kujiletea maendelea kwa kushirikiana na Serikali yao ni pamoja na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu”. Amesema zipo njia mbalimbali za kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kipindi hiki kutoa taarifa sahihi ni jukumu namba moja ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi. 

Sensa ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya kwanza nchini kote na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa mara moja tu.
=30=

No comments:

Post a Comment