Wednesday, November 23, 2011

RC AKEMEA UKATAJI MITI OVYO

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameagiza kuacha tabia ya kukata miti ovyo ili kuunusuru Mkoa na kugeuka jangwa kama baadhi ya maeneo ambayo yanakubwa na ukame wa mara kwa mara na kusababisha upungufu wa chakula.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa Kata ya Idodi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa alipofanya ziara ya kuhamasisha shughuli za kilimo na elimu.
Dk. Ishengoma amesema kuwa katika kipindi cha kuandaa mashamba wananchi wamekuwa na tabia ya kukata miti katika mashamba yao. Amesema “msikate miti yote sababu miti hii ndiyo inayotengeneza mvua hivyo, tukiendelea kukata miti hiyo ukame hautaisha bali utazidi kuongezeka katika eneo kubwa zaidi”.
Kutokana na ukame wa mara kwa mara unaosababisha upungufu wa chakula, Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na upungufu wa chakula ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha mtama amesema Dk. Ishengoma.
Amesema ni vizuri wananchi wakabadili mawazo ya kutegemea mazao ya mahindi na mpunga pekee na kufikiria kilimo cha zao la mtama.
Akiongelea vocha za pembejeo za kilimo, amesema kuwa wananchi waliopata vocha hizo wazitumie vizuri ili kuweza kunufaika nazo na kufikiwa kwa malengo ya serikali ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia kilimo. Amesema wananchi wanawajibu wa kufahamu kuwa seti moja ya vocha za pembejeo inahusisha mbolea ya kupandia, mbegu bora na mbolea ya kukuzia.
Aidha, alitahadharisha kwa mawakala wasiowaaminifu kuwa lazima wafuate utaratibu uliowekwa katika usambazaji na matumizi ya vocha hizo na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wakala yeyote atakayekiuka utaratibu uliowekwa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa anafanya ziara ya kuhamasisha kilimo na elimu baada ya msimu wa kilimo kuanza wakati baadhi ya sehemu katika Tarafa ya Idodi ni miongoni mwa maeneo yaliyokubwa na ukame na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa anafanya ziara ya kuhamasisha kilimo na elimu baada ya msimu wa kilimo kuanza wakati baadhi ya sehemu katika Tarafa ya Idodi ni miongoni mwa maeneo yaliyokubwa na ukame na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula. 

RC AHIMIZA MAZAO YANAYOSTAHIMILI UKAME


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa Tarafa ya Idodi kufikiria kilimo cha mazao yanayostahimili ukame ili kukabiliana na tatizo la njaa linalowakabili wananchi wa Tarafa hiyo mara kwa mara.
Dk. Christine anayefanya ziara maalumu ya kuhamasisha shughuli za kilimo na elimu katika Mkoa wa Iringa, siku yake ya kwanza ya ziara aliyoifanya katika Kata ya Nzihi, Tungamalenga na Mahuninga amesisitiza kilimo cha zao la mtama pamoja na mazao mengine. Amesema “si lazima kulima mahindi na mpunga tu kama zao la chakula, bali tubadilishe kidogo fikra ili tuweze kulima mazao yanayostahimili ukame na tuanze na zao la mtama”.
Amesema pamoja na jitihada za Serikali ya Mkoa kuhimiza kilimo cha zao la mtama lakini mkulima mmoja mmoja ni vizuri akalima pia muhogo na viazi vitamu kwa kujihakikishia uhakika na hifadhi ya chakula.
Amesema kuwa matarajio ni kila kaya kulima angalau ekari mbili za mtama. Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, itazigawa hizo mbegu bure kwa wakulima na kuwakumbusha wakulima kuwa wamebakiwa na kazi moja tu ya kulima baada ya kuondolewa gharama za kununua mbegu ya mtama. Vilevile, amesisitiza kuwa serikali itakuwa makini katika kuzigawa mbegu hizo kwa kuangalia eneo lililolimwa ili kuepukana na baadhi ya wakulima kuzitumia kwa matumizi mengine tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na serikali.
Aidha, amewataka wananchi kujihusisha na ufugaji wa wanyama wadogo wadogo kama kuku, bata na mbuzi ili uweze kuwasidia katika kukidhi mahitaji ya kawaida ya nyumbani. Amesema “ufugaji wa wanyama wadogowadogo unasaidia sana hasa akina mama kuweza kukidhi mahitaji ya familia”.
Akiongelea ufugaji wa ng’ombe ameshauri kuwa yatumike madume bora ili kupata maziwa mengi. Vilevile ameshauri kutumia njia ya uhamilishaji ili kupunguza gharama za ufugaji wa madume mengi ya ng’ombe na uhifadhi wa mazingira.
Kuhusu elimu, Mkuu wa Mkoa ameagiza watoto wote watakaofaulu wapelekwe shule ili kukuza kuwango cha elimu katika Mkoa. Amesema “kila mmoja lazima aone fahari kumpeleka mwanae shule na hasa watoto wa kike ili kuachana na tamaduni za kale zilizokuwa zikimfanya mtoto wa kike kukosa elimu”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa anafanya ziara ya kuhamasisha kilimo na elimu baada ya msimu wa kilimo kuanza wakati baadhi ya sehemu katika Tarafa ya Idodi ni miongoni mwa maeneo yaliyokubwa na ukame na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula. 
=30=