Monday, November 26, 2012

UKATILI WA KIJINSIA...WANAUME WAWAJIBIKE



Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa nchini kutokana na baadhi ya dhana na mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka na kuwanyima wanawake haki zao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake wakati wa uzinguzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia maadhimisho yaliyofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa Manispaa ya Iringa.

Dkt. Christine amesema “unyanyasaji wa kijinsia unaweza kutokea kwa jinsi yeyote ile, mwanamke, mwanaume au watoto. Ila huwapata sana kina mama na vijana hasa watoto wa kike. Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa ulimwenguni kote, nchini Tanzania, kadhalika katika mikoa yetu ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi”. Amesema kuwa baadhi ya dhana kama umasikini, mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka na kuwanyima wanawake haki zao ni moja klati ya viini vinavyopelekea unyanyasaji wa kijinsia nchini. Amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tanzania Demographic Health Survey mwaka 2010, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakuwango cha wastani wa vitendo unyanyasaji wa kijinsia. Amesema “Iringa 54%, Ruvuma 55%, Mbeya 55%, Mtwara 26%, Lindi 22% na Rukwa 56%” amesema kuwa kwa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa wastani wa kiwango ni mkubwa ukilinganisha na na kiwango cha wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 44.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa katika kupambana na hali hiyo, Serikali kupitia Mpango wa kupambana na Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA), mabadiliko ya Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, imefanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia. Aidha, amesema kuwa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau utaendelea kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali ili waweze kutatua na kuzifanyia kazi kesi zinazohusi ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa jitihada hizo, Mkuu wa Mkoa amezitaja kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi na kusisitiza kuwa wananchi wahamasishwe kwenda kutoa taarifa, kuhakikishiwa usalama wao na kuamini kuwa madawati yale yako kwa ajili yao. Amesema katika kuliwekea mkazo tatizo hilo, Mkoa umeziagiza Halmashauri kuendelea kutenga bajeti katika mipango yao kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, haki za binadamu, sheria na madhara yatokanayo na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Dkt. Christine amesema “yatupasa tukumbuke kuwa ukatili wa kijinsia sio suala la wanawake ama watoto pekee. Ni muhimu sana kwa wakati huu; hasa kwa kina baba kuwa chachu ya mabadiliko kwa kupinga vitendo vya ukatili na hata kukemea tabia hizo”. Amesema ni vema viongozi na jamii ikatumia ushawishi wake kuamsha majadiliano juu ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, kuvipinga kwa nguvu zote na kuwa mfano bora wa kuigwa ili kuimarisha ustawi wa nchi ya Tanzania.
=30=

MUFINDI WAJIDHATITI KUFIKISHA PEMBEJEO VIJIJINI




Wilaya ya Mufindi imehakikisha usambazaji wa pembejeo unafanikiwa kwa kuhakikisha mbadala wa mawakala waliopungukiwa na uwezo wa kusambaza pembejeo za kukuzia baada ya kutoa taarifa kwa uongozi wa wilaya na wakala mwingine kuendeleza usambazaji huo haraka ili kutokuwachelewesha wakulima.

Hayo yamesemwa na Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Mufindi, Edna Kaduma wakati akiwasilisha taarifa ya usambazaji wa pembejeo kwa wilaya ya Mufindi mwaka 2011/2012 na 2012/2013 katika kikao cha kamati ya vocha ya mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Edna amesema kuwa miongoni mwa changamoto ilikuwa ni mawakala kupungukiwa uwezo wa kusambaza pembejeo hasa wakati ilipoanza kutumika mbolea ya kukuzia. Amesema kuwa mawakala hao walitoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya na haraka walipatikana mawakala wengine kwa lengo la kuendeleza huduma hiyo pasipo kuwachelewesha wakulima kutumia mbolea hiyo ya kukuzia. Amesema katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, kamati ya vocha Wilaya ya Mufindi ilifanya mikutano mitatu na mawakala wote kwa lengo la kutathmini uwezo wa kila mmoja na kukubaliana maeneo ya kuhudumia kulingana na uwezo wa kila wakala aidha, wale wenye uwezo mkubwa walikubali kutoa huduma kwa maeneo yaliyokosa mawakala.   

Amesema ili kuweka uwazi katika mchakato huo, kamati ya vocha ya wilaya ilifanya mikutano ya hadhara na wananchi kwa kila kata na pamoja na kukutana na kamati za vocha za vijiji kwa ajili ya kutoa maelekezo ya utaratibu wa mpito wa usambazaji wa pembejeo kwa kutumia vocha. Amesema miongoni mwa changamoto ni kupanda kwa bei za pembejeo baadhi ya wakulima wameshindwa kutumia pembejeo bora. Amesema miongoni mwa changamoto pia ni kupungua kwa wanufaika kutokana na kupungua kwa idadi ya vocha na kuchelewa kuwa vocha za ruzuku kusababisha baadhi ya vijiji kutotumia vocha za mbegu bora.

Edna amesema kuwa ili kuhakikisha usambazaji unafika katika maeneo yote suala la mawasiliano lilipewa uzito unaostahili. Amesema mawasiliano na ufuatiliaji wa mara kwa mara ulifanyika kati ya wilaya na vijiji ili kuhakikisha maeneo yote usambazaji unakwenda vizuri na pembejeo zinauzwa kwa bei iliyokubalika katika vikao.

Akiongelea maadalizi ya pembejeo kwa msimu wa mwaka 2012/2013, Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wilaya ya Mufindi amesema kuwa mahitaji ya mbolea kwa wilaya ya Mufindi, jumla ya tani 13,720 na mahitaji ya mbegu ni jumla ya tani 887. Amesema “msimu huu wilaya imepokea mgao wa vocha seti 22,188 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mgao wa msimu uliopita.
=30=