Wilaya ya Mufindi
imehakikisha usambazaji wa pembejeo unafanikiwa kwa kuhakikisha mbadala wa
mawakala waliopungukiwa na uwezo wa kusambaza pembejeo za kukuzia baada ya
kutoa taarifa kwa uongozi wa wilaya na wakala mwingine kuendeleza usambazaji
huo haraka ili kutokuwachelewesha wakulima.
Hayo yamesemwa na
Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Mufindi, Edna Kaduma wakati
akiwasilisha taarifa ya usambazaji wa pembejeo kwa wilaya ya Mufindi mwaka
2011/2012 na 2012/2013 katika kikao cha kamati ya vocha ya mkoa kilichofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Edna amesema kuwa
miongoni mwa changamoto ilikuwa ni mawakala kupungukiwa uwezo wa kusambaza
pembejeo hasa wakati ilipoanza kutumika mbolea ya kukuzia. Amesema kuwa
mawakala hao walitoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya na haraka walipatikana
mawakala wengine kwa lengo la kuendeleza huduma hiyo pasipo kuwachelewesha
wakulima kutumia mbolea hiyo ya kukuzia. Amesema katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, kamati
ya vocha Wilaya ya Mufindi ilifanya mikutano mitatu na mawakala wote kwa lengo
la kutathmini uwezo wa kila mmoja na kukubaliana maeneo ya kuhudumia kulingana
na uwezo wa kila wakala aidha, wale wenye uwezo mkubwa walikubali kutoa huduma
kwa maeneo yaliyokosa mawakala.
Amesema ili
kuweka uwazi katika mchakato huo, kamati ya vocha ya wilaya ilifanya mikutano
ya hadhara na wananchi kwa kila kata na pamoja na kukutana na kamati za vocha
za vijiji kwa ajili ya kutoa maelekezo ya utaratibu wa mpito wa usambazaji wa
pembejeo kwa kutumia vocha. Amesema miongoni mwa changamoto ni kupanda kwa bei
za pembejeo baadhi ya wakulima wameshindwa kutumia pembejeo bora. Amesema
miongoni mwa changamoto pia ni kupungua kwa wanufaika kutokana na kupungua kwa
idadi ya vocha na kuchelewa kuwa vocha za ruzuku kusababisha baadhi ya vijiji
kutotumia vocha za mbegu bora.
Edna amesema kuwa
ili kuhakikisha usambazaji unafika katika maeneo yote suala la mawasiliano
lilipewa uzito unaostahili. Amesema mawasiliano na ufuatiliaji wa mara kwa mara
ulifanyika kati ya wilaya na vijiji ili kuhakikisha maeneo yote usambazaji
unakwenda vizuri na pembejeo zinauzwa kwa bei iliyokubalika katika vikao.
Akiongelea
maadalizi ya pembejeo kwa msimu wa mwaka 2012/2013, Afisa Kilimo, Mifugo na
Ushirika wilaya ya Mufindi amesema kuwa mahitaji ya mbolea kwa wilaya ya
Mufindi, jumla ya tani 13,720 na mahitaji ya mbegu ni jumla ya tani 887. Amesema
“msimu huu wilaya imepokea mgao wa vocha seti 22,188 ikiwa ni pungufu kwa
asilimia 50 ikilinganishwa na mgao wa msimu uliopita.
=30=
No comments:
Post a Comment