Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa nchini
kutokana na baadhi ya dhana na mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka
na kuwanyima wanawake haki zao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma katika hotuba yake wakati wa uzinguzi wa kampeni ya siku 16
za kupinga unyanyasaji wa kijinsia maadhimisho yaliyofanyika katika uwanja wa
Mwembetogwa Manispaa ya Iringa.
Dkt. Christine amesema “unyanyasaji wa kijinsia
unaweza kutokea kwa jinsi yeyote ile, mwanamke, mwanaume au watoto. Ila
huwapata sana kina mama na vijana hasa watoto wa kike. Unyanyasaji wa kijinsia
ni changamoto kubwa ulimwenguni kote, nchini Tanzania, kadhalika katika mikoa
yetu ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi”. Amesema kuwa
baadhi ya dhana kama umasikini, mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka
na kuwanyima wanawake haki zao ni moja klati ya viini vinavyopelekea
unyanyasaji wa kijinsia nchini. Amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
Tanzania Demographic Health Survey mwaka 2010, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
inakuwango cha wastani wa vitendo unyanyasaji wa kijinsia. Amesema “Iringa 54%,
Ruvuma 55%, Mbeya 55%, Mtwara 26%, Lindi 22% na Rukwa 56%” amesema kuwa kwa
mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa wastani wa kiwango ni mkubwa
ukilinganisha na na kiwango cha wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 44.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa katika kupambana
na hali hiyo, Serikali kupitia Mpango wa kupambana na Umasikini na Kukuza
Uchumi Tanzania (MKUKUTA), mabadiliko ya Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo
Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, imefanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo la
ukatili wa kijinsia. Aidha, amesema kuwa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na
wadau utaendelea kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali
ili waweze kutatua na kuzifanyia kazi kesi zinazohusi ukatili wa kijinsia.
Miongoni mwa jitihada hizo, Mkuu wa Mkoa amezitaja
kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya
polisi na kusisitiza kuwa wananchi wahamasishwe kwenda kutoa taarifa,
kuhakikishiwa usalama wao na kuamini kuwa madawati yale yako kwa ajili yao.
Amesema katika kuliwekea mkazo tatizo hilo, Mkoa umeziagiza Halmashauri
kuendelea kutenga bajeti katika mipango yao kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu
unyanyasaji wa kijinsia, haki za binadamu, sheria na madhara yatokanayo na
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Dkt. Christine amesema “yatupasa tukumbuke kuwa
ukatili wa kijinsia sio suala la wanawake ama watoto pekee. Ni muhimu sana kwa
wakati huu; hasa kwa kina baba kuwa chachu ya mabadiliko kwa kupinga vitendo
vya ukatili na hata kukemea tabia hizo”. Amesema ni vema viongozi na jamii
ikatumia ushawishi wake kuamsha majadiliano juu ya vitendo hivyo vya ukatili wa
kijinsia, kuvipinga kwa nguvu zote na kuwa mfano bora wa kuigwa ili kuimarisha
ustawi wa nchi ya Tanzania.
=30=
No comments:
Post a Comment