Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mafunzo
elekezi ya awali kwa watumishi wapya katika ofisi ya mkuu wa mkoa Iringa yataleta
mabadiliko chanya katika utumishi wa umma mkoani Iringa.
Kauli
hiyo ilitolewa na Afisa Takwimu katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Iringa,
Hildegarda Kimaro katika mahojiano maalum yaliyofanyika katika hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Iringa jana.
Kimaro
alisema “mafunzo elekezi ya awali kwa
watumishi wapya ni mazuri, tumejifunza mambo mbalimbali ambayo hatukuyafahamu
awali. Mfano sheria ya utumishi wa umma na kanuni zake na utunzaji wa
kumbukumbu”.
Aliongeza kuwa awali utunzaji kumbukumbu lilifahamika kuwa ni
jukumu la watunza kumbukumbu wasaidizi katika ofisi ya mkuu wa mkoa, lakini
baada ya mafunzo imebainika kuwa utunzaji kumbukumbu ni jukumu wa watumishi
wote wa umma kwa nafasi zao.
Akiongelea
umuhimu wa mafunzo hayo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma, Kimaro alisema
kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutokuvunja sheria za utumishi. “Mafunzo haya ni muhimu na yatatusaidia
kutokuvunja sheria ambazo tungevunja bila kufahamu. Kwa mafunzo haya tumeweza
kufahamu jambo ambalo ni sahihi kufanya katika utumishi wa umma na ambayo si
sahihi kufanya katika utumishi wa umma” alisema Kimaro.
Kimaro
alishauri kuwa watumishi wapya wanapoajiriwa wapewe mafunzo elekezi ya awali angalau
ndani ya miezi mitatu ya awali.
“Katika
kuongeza umakini wa mafunzo, ni vizuri mafunzo hayo yakatolewa nje ya eneo la
kazi ili kuwawezesha washiriki wa mafunzo kujikita katika mafunzo kuliko
kutekeleza majukumu mengine ya kiutumishi jambo linaloathiri utulivu na usikivu
wakati wa mafunzo” alishauri Kimaro.
Mafunzo elekezi ya awali ya siku tano kwa
watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa
kushirikiana na chuo cha utumishi wa umma (TPSC) yakishirikisha watumishi wapya
107 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi za wakuu wa wilaya na hospitali ya
rufaa ya mkoa.
=30=