Wednesday, September 13, 2017

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA NIDHAMU IRINGA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Watumishi wa umma mkoani Iringa wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao wanapowahudumia wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa umma walioajiliwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa, mafunzo yalifanyika katika ukumbi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa jana.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu akiongea na watumishi wapya, kulia ni Katibu Tawala Msaidi Utawala, Lucas Kambelenje (kulia) kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dr Robert Salim

Ayubu alisema kuwa msingi wa utumishi wa umma umejikita katika uadilifu, hivyo mtumishi wa umma lazima afanye kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr John Magufuli imejipambanua kwa kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma. 

Aliwataka watumishi wa umma mkoani Iringa kuwa mfano mzuri wa kuingwa katika nidhamu na uwajibikaji wanapowahudumia wananchi ili wabaki na kumbukumbu ya huduma njema.

Akiongelea umuhimu wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma, Katibu Tawala mkoa alisema kuwa watumishi wengi wanatoka katika maeneo tofauti yenye mitazamo tofauti hivyo, kuitaji kufundishwa utaratibu wa kazi katika serikali. 

Mafunzo haya ni muhimu sana unapoingia katika utumishi wa umma. Tunatoka katika vyuo tofauti na tamaduni tofauti hivyo, hata tabia zinakuwa tofauti. Mafunzo haya yanalenga kutufundisha namna utumishi wa umma ulivyo na jinsi mtumishi wa umma anavyotakiwa kuonekana na kutenda kazi” alisema Ayubu.

Aliwataka watumishi hao kubadilika baada ya mafunzo kimtazamo na kiutendaji na kuzingatia viwango vya juu katika utumishi wao. “Unajua unapoingia katika utumishi wa umma, unajikuta unafanya makosa, ila tunashindwa kukuchukulia hatua za kiutumishi badala yake tunalazimika kukufanyia ushauri zaidi

Tunabadilika na kuwa wazazi na walezi katika kuwaelimisha watumishi” alisema Ayubu. Aliongeza kuwa baada ya mafunzo haya watakuwa wakiwachukulia hatua stahili za kiutumishi watumishi wote watakaotenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Alisema kuwa katika mafunzo hayo watumishi wa umma watafundishwa muundo wa serikali, uendeshaji wa shughuli za serikali, utunzaji wa kumbukumbu, maadili ya utumishi wa umma, maboresho ya utumishi wa umma, huduma kwa mteja, sheria ya utumishi wa umma namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake, mpango wa kudhibiti ukimwi kwa watumishi wa umma na upimaji wa wazi utendaji kazi kwa watumishi wa umma.

Mafunzo elekezi ya awali ya siku tano kwa watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na chuo cha utumishi wa umma (TPSC) yakishirikisha watumishi wapya 107 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi za wakuu wa wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa.
=30=

IRUWASA YAPONGEZWA KUTENGA SIKU YA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Iringa mjini (IRUWASA) imepongezwa kwa utekelezaji wa agizo la mkuu wa mkoa wa Iringa la kutenga siku ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero na malalamiko ya wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipotembelea Iruwasa kukagua utekelezaji wa agizo lake mkoani Iringa.
Afisa Uhusiano IRUWASA Restituta Sakila (kushoto) akimuonesha jambo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipotembelea taasisi hiyo kukagua wanavyopokea na kusikiliza Malalamiko ya wananchi

Nianze kwa kuwapongeza IRUWASA kwa kazi nzuri mnayofanya kupokea na kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi. Mheshimiwa Rais Dr John Magufuli amekuwa akipokea barua nyingi za malalamiko ya wananchi. Malalamiko mengine ni madogo madogo ambayo sisi wasaidizi wake tunaweza kuyatatua. Ni matarajio ya mheshimiwa Rais kuona kero na malalamiko yote ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi. Hili mnalotekeleza IRUWASA ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya mheshimiwa Rais” alisema mheshimiwa Masenza.

Akiongelea changamoto ya upotevu wa maji inayowakabili wananchi wengi wanaohudumiwa na IRIWASA, mkuu wa mkoa aliwataka kuweka utaratibu maalum wa kupitia miundombinu ya mtandao wa mabomba ili kujiridhisha na uimara wake. Aidha, aliwataka IRUWASA kutafuta ufumbuzi wa mita za maji za malipo kabla ya huduma ya maji ambazo wateja wengi wametokea kuzipenda.

Katika taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa IRUWASA, Gilbert Kayange kwa mkuu wa mkoa wa Iringa kuhusu usikilizaji na utatuzi wa kero na malalamiko ya wananchi alisema kuwa, jumla ya wananchi 79 waliwasilisha kero na mlalamikoa yao. 

Kati ya kero na malalamiko 79 yaliyowasilishwa, 71 yalipatiwa ufumbuzi na wananchi kuridhika. Kero nane tunaendelea kuzishughulikia ambazo ni wananchi kuhitaji huduma ya kuunganishwa na mtandao wa maji” alisema Kayange.

Kayange alisema kuwa IRUWASA imefanikiwa kufikisha huduma ya maji kwa 96% ya wakazi wa Manispaa ya Iringa. Aliongeza kuwa mamlaka yake inaendelea kushughulikia tatizo la kufikisha huduma ya maji katika maeneo ya Kitwiru, Igumbilo na Isakalilo.

Mkurugenzi mtendaji wa IRIWASA, alisema kuwa 90% ya malalamiko ya wananchi yanatokana na ukubwa wa bili za maji na mivujo ya maji. Aliongeza kuwa awali wananchi walikuwa wakifanyiwa tathmini ya vifaa na wananchi kununua vifaa wenyewe jambo lililosababisha ununuzi wa vifaa vilivyo chini ya kiwango na kuchangia katika uvujaji wa maji. 

Alitaja changamoto ya mita za huduma ya malipo kabla kuwa zinapendwa na wateja wengi zaidi na mamlaka haina uwezo wa kuwafungia wateja wote na kusababisha mita hizo kufungwa kimkakati.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo lake kwa taasisi za umma kutenga siku maalum ya akusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi. Katika siku yake ya kwanza alitembelea taasisi za IRUWASA, TANESCO, TRA na Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Iringa.
=30=

OFISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTENGA SIKU YA KUSIKILIZA MALALAMIKO YA WANANCHI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Ofisi za serikali mkoani Iringa zimetakiwa kutenga siku maalum kwa ajili ya kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kutafuta ufumbuzi wake.

Agizo hilo lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza baada ya kutembelea ofisi za TANESCO, IRUWASA, TRA na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Iringa kujiridhisha na utekelezaji wa agizo lake la kutenga siku moja kwa wiki kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa wananchi wanakero na malalamiko mengi yanayokwamisha mustakabari wao wa kila siku. Kero na malalamiko hayo yamekuwa yakiwakwamisha kutekeleza majukumu yao ya kila siku na wakati mwingine kuishia kuilalamikia serikali iliyo madarakani. 

Kwa kuwa nchi yetu inafuata misingi ya utawala bora na utawala wa sheria, uliojikita katika kutoa huduma bora kwa wananchi, niliziagiza ofisi za umma mkoani Iringa kutenga siku maalum ya kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kuitangaza siku hiyo ili wananchi waifahamu” alisema mheshimiwa Masenza. 

Katika kufanikisha agizo hilo, Mkuu wa Mkoa amezitaka ofisi za umma kuunda kamati kwa ajili ya kupokea na kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu na kutoa mrejesho kwa wananchi walalamikaji. 

Upokeaji na usikilizaji wa kero na malalamiko ya wananchi uende sambamba na kuorodhesha kero na malalamiko hayo katika daftari la kudumu likionesha jina la mlalamikaji, aina ya lalamiko, afisa aliyepokea lalamiko husika, tarehe ya kupokea na kulitatua, mrejesho na maoni” alisisitiza mheshimiwa Masenza.

Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa imetenga siku ya jumatatu ya kila wiki ya kazi kwa ajili ya kupokea, kusikiliza na kutatua ufumbuzi wa kero na malalamiko ya wananchi.
=30=

VYOMBO VYA HABARI VYATAKIWA KUTANGAZA UTALII KARIBU KUSINI



Na Mwandishi Maalum, Iringa
Vyombo vya habari katika mikoa ya nyanda za juu kusini vimetakiwa kutangaza maandalizi ya maonesho ya Utalii Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda ili kuwaletea maendeleo wananchi wa kanda hiyo.

Wito huo ulitolewa na mwenyekiti wa kikao cha viongozi wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini katika maandalizi ya maadhimisho ya maonesho ya Utalii Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO), mheshimiwa Amina Masenza katika kikao kilichofanyika hifadhi ya taifa ya Ruaha jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Mheshiniwa Masenza ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa vyombo vya habari katika mikoa ya nyanda za juu kusini vina mchango mkubwa katika kufanikisha maonesho ya Utalii Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO). 

Waandishi wa habari mna jukumu muhimu katika kufanikisha shughuli hii. Nawaomba mtusaidie kutangaza Utalii Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo” alisema mheshimiwa Masenza.

Wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini walioshiri ziara hiyo ni mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Songwe na mkuu wa mkoa wa Njombe.

Maonesho ya Utalii yatafanyika pamoja na Maonesho shughuli za Viwanda Vidogo (SIDO) kanda ya nyanda za juu kusini kwa Mwaka 2017.  Maonesho haya yamepangwa kufanyika kuanzia tarehe 29/09/2017 hadi tarehe 02/10/2017.
=30=

KARIBU KUSINI NA SIDO KULETA WANYAMAPORI HAI MAONESHO YA IRINGA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Kamati ya maandalizi ya maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kanda ya nyanda za juu kusini imetakiwa kuhakikisha wanyamapori hai wanakuwepo katika maonesho hayo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha pamoja cha viongozi wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini cha maandalizi ya maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kanda ya nyanda z juu kusini kilichofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha nje kidogo ya mji wa Iringa.
Picha ya pamoja na wakuu wa Mikoa na watalaam katika Hifadhi ya taifa ya Ruaha

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa wanyamapori hai ni muhimu katika maonesho hayo kwa sababu wananchi wengi wanapenda kuwaona wanyamapori hai moja kwa moja. Aidha, alishauri kasi ya kufuatilia wanyamapori hao inayofanywa baina ya kamati ya maandalizi na wizara ya Maliasili na Utalii iongezwe.

Katika taarifa ya kamati ya maandalizi iliyowasilishwa na Fikira Kisimba alisema kuwa ufuatiliaji unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kupata wanyama hao. “Wizara imetoa bajeti elekezi ambapo mikoa inawajibika kuchangia jumla ya shilingi 4,000,000 kukodi mabanda yote manne ya wanyama” alisema Kisimba. 

Akiongelea wadau waliothibitisha kushiriki katika maonesho hayo, alisema kuwa wadau 312 wamethibitisha kushiriki. Aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni wizara ya Maliasili na Utalii; wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezeji; wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; na TATO. Wengine ni KILI FAIR; Wakala wa Misitu Tanzania; Ngonga beach; UPL Link Mbeya; Uyole cultural Enterprises; Baraza la Biashara la Taifa; Heifer International; Care International na Wajasiliamali 300.

Wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini walioshiri ziara hiyo ni Amina Masenza mkuu wa Mkoa wa Iringa, Luteni (Mst) Chiku Galawa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Christopher Ole Sendeka mkuu wa mkoa wa Njombe.

Maonesho ya Utalii yatafanyika pamoja na Maonesho shughuli za Viwanda Vidogo (SIDO) kanda ya nyanda za juu kusini kwa Mwaka 2017.  Maonesho haya yamepangwa kufanyika kuanzia tarehe 29/09/2017 hadi tarehe 02/10/2017.
=30=