Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka
ya majisafi na usafi wa mazingira Iringa mjini (IRUWASA) imepongezwa kwa
utekelezaji wa agizo la mkuu wa mkoa wa Iringa la kutenga siku ya kusikiliza na
kutafuta ufumbuzi wa kero na malalamiko ya wananchi.
Pongezi
hizo zimetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza
alipotembelea Iruwasa kukagua utekelezaji wa agizo lake mkoani Iringa.
Afisa Uhusiano IRUWASA Restituta Sakila (kushoto) akimuonesha jambo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipotembelea taasisi hiyo kukagua wanavyopokea na kusikiliza Malalamiko ya wananchi |
“Nianze kwa kuwapongeza IRUWASA kwa kazi
nzuri mnayofanya kupokea na kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi.
Mheshimiwa Rais Dr John Magufuli amekuwa akipokea barua nyingi za malalamiko ya
wananchi. Malalamiko mengine ni madogo madogo ambayo sisi wasaidizi wake
tunaweza kuyatatua. Ni matarajio ya mheshimiwa Rais kuona kero na malalamiko
yote ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi. Hili mnalotekeleza IRUWASA ni sehemu ya
utekelezaji wa dhamira ya mheshimiwa Rais” alisema mheshimiwa Masenza.
Akiongelea
changamoto ya upotevu wa maji inayowakabili wananchi wengi wanaohudumiwa na IRIWASA,
mkuu wa mkoa aliwataka kuweka utaratibu maalum wa kupitia miundombinu ya
mtandao wa mabomba ili kujiridhisha na uimara wake. Aidha, aliwataka IRUWASA kutafuta
ufumbuzi wa mita za maji za malipo kabla ya huduma ya maji ambazo wateja wengi
wametokea kuzipenda.
Katika
taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa IRUWASA, Gilbert Kayange kwa mkuu wa mkoa wa
Iringa kuhusu usikilizaji na utatuzi wa kero na malalamiko ya wananchi alisema
kuwa, jumla ya wananchi 79 waliwasilisha kero na mlalamikoa yao.
“Kati ya kero na malalamiko 79
yaliyowasilishwa, 71 yalipatiwa ufumbuzi na wananchi kuridhika. Kero nane
tunaendelea kuzishughulikia ambazo ni wananchi kuhitaji huduma ya kuunganishwa
na mtandao wa maji” alisema Kayange.
Kayange
alisema kuwa IRUWASA imefanikiwa kufikisha huduma ya maji kwa 96% ya wakazi wa
Manispaa ya Iringa. Aliongeza kuwa mamlaka yake inaendelea kushughulikia tatizo
la kufikisha huduma ya maji katika maeneo ya Kitwiru, Igumbilo na Isakalilo.
Mkurugenzi
mtendaji wa IRIWASA, alisema kuwa 90% ya malalamiko ya wananchi yanatokana na
ukubwa wa bili za maji na mivujo ya maji. Aliongeza kuwa awali wananchi
walikuwa wakifanyiwa tathmini ya vifaa na wananchi kununua vifaa wenyewe jambo
lililosababisha ununuzi wa vifaa vilivyo chini ya kiwango na kuchangia katika
uvujaji wa maji.
Alitaja changamoto ya mita za huduma ya malipo kabla kuwa zinapendwa
na wateja wengi zaidi na mamlaka haina uwezo wa kuwafungia wateja wote na
kusababisha mita hizo kufungwa kimkakati.
Mkuu
wa mkoa wa Iringa, yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo lake kwa
taasisi za umma kutenga siku maalum ya akusikiliza kero na malalamiko ya
wananchi na kuyatafutia ufumbuzi. Katika siku yake ya kwanza alitembelea
taasisi za IRUWASA, TANESCO, TRA na Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Iringa.
=30=
No comments:
Post a Comment