Wednesday, September 13, 2017

HIFADHI YA RUAHA YAATHIRIWA NA KUKAUKA KWA MTO RUAHA MKUU



Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Hifadhi ya taifa ya Ruaha inaathiriwa na changamoto ya kukauka kwa mto Ruaha mkuu jambo linalohatarisha maisha ya wanyama na uendelevu wa hifadhi hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa na kaimu mkuu wa hifadhi ya Ruaha, Halima Kiwango alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hifadhi ya taifa ya Ruaha kwa wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini waliotembelea hifadhi hiyo na kufanya kikao cha pamoja cha maandalizi ya Utalii Karibu Kusini hifadhini hapo.

Kiwango alisema kuwa changamoto kwa uhifadhi ni kukauka kwa mto Ruaha mkuu jambo linalohatarisha uhai wa wanyama katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Akiongelea sababu za kukauka kwa mto Ruaha mkuu, Kiwango alizitaja kuwa ni kilimo cha umwagiliaji mashamba makubwa na madogo ya mpunga katika bonde la mto Ruaha mkuu. Sababu nyingine alizitaja kuwa ni ongezeko la mifugo katika bonde la Usangu na watumia maji katika bonde hilo. Nyingine ni uvamizi wa wanyamapori katika maeneo ya nje ya hifadhi na ujangili wa Tembo.
Mhifadhi Halima Kiwango

Kaimu mkuu wa hifadhi ya taifa ya Ruaha alizitaja changamoto nyingine kuwa ni barabara kuu kutoka Iringa hadi lango kuu la kuingia hifadhi ya Ruaha kutokuwa ya kiwango cha lami inachangia idadi ndogo ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo. 

Kutokuwa na lango la kuingilia hifadhini upande wa Usangu kumekuwa kukisababisha watalii wengi kutokufika katika hifadhi ya Ruaha. Changamoto nyingine ni hifadhi bado haijajulikana sana kwa watalii wa nje na ndani” alisema Kiwango.
=30=

No comments:

Post a Comment