Na
Mwandishi Maalum, IRINGA
Kamati ya maandalizi ya Utalii Karibu
Kusini imeunda kamati ndogo za ufuatiliaji na usimamizi wa kufanikisha maadhimisho
ya siku ya Utalii Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo kanda
ya nyanda za juu kusini.
Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa
kamati ya maandalizi, Fikira Kisimba alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maandalizi
ya maadhimisho ya siku ya Utalii Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za
viwanda vidogo kanda ya nyanda za juu kunisi kwa viongozi wakuu wa mikoa nyanda
za juu kusini walipotembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha na kufanya kikao cha
pamoja katika hifadhi hiyo iliyopo nje kidogo ya mji wa Iringa.
Kisimba alisema kuwa katika kufanikisha
maonesho hayo, kamati ya maandalizi imefanya shughuli mbalimbali pamoja na
kuunda kamati ndogondogo. Kamati zilizoundwa alizitaja kuwa ni kamati ya
Mipango na Fedha; Kamati ya Mapokezi, Usafiri na Malazi; Kamati ya Chakula,
Afya na usafi wa Mazingira.
Nyingine ni Kamati ya Miundombinu na Mapambo;
Kamati ya Ulinzi na Usalama; Habari na Uenezi na Kongamano na Maonesho ya nje.
Kisimba aliongeza kuwa kamati hizo saba zimeundwa kwa kushirikisha sekta
binafsi na sekta ya umma ili kutoa uwiano sawia.
Akiongelea uhamasishaji wa jamii na
mialiko, mwenyekiti huyo wa maandalizi alisema kuwa uhamasishaji unaendelea
kufanyika kwa wadau mbalimbali. Alisema kuwa ofisi za SIDO katika mikoa ya
nyanda za juu kusini imekwisha wataarifu wajasiriamali waliopo katika mikoa
yao. Wadau wakubwa 51 wameandikiwa barua za kuomba michango na ushiriki.
“Taarifa ya mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa
wakati wa Maonesho ya Nane Nane - Mbeya kwa kushirikiana na Wakuu wa Wilaya na
Katibu Tawala Mkoa; Vikao mbalimbali vya Maandalizi na vikao vingine vya wadau
vinavyofanyika na kushirikisha vyombo
vya Habari” alisema Kisimba.
Wakuu
wa mikoa ya nyanda za juu kusini walioshiri ziara hiyo ni Amina Masenza mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Luteni (Mst) Chiku Galawa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Christopher
Ole Sendeka mkuu wa mkoa wa Njombe.
Maonesho
ya Utalii yatafanyika pamoja na Maonesho shughuli za Viwanda Vidogo (SIDO)
kanda ya nyanda za juu kusini kwa Mwaka 2017.
Maonesho haya yamepangwa kufanyika kuanzia tarehe 29/09/2017 hadi tarehe
02/10/2017.
=30=
No comments:
Post a Comment