Na.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Ofisi
za serikali mkoani Iringa zimetakiwa kutenga siku maalum kwa ajili ya
kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kutafuta ufumbuzi wake.
Agizo
hilo lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza baada ya
kutembelea ofisi za TANESCO, IRUWASA, TRA na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Iringa
kujiridhisha na utekelezaji wa agizo lake la kutenga siku moja kwa wiki
kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi.
Mheshimiwa Masenza
alisema kuwa wananchi wanakero na malalamiko mengi yanayokwamisha mustakabari
wao wa kila siku. Kero na malalamiko hayo yamekuwa yakiwakwamisha kutekeleza
majukumu yao ya kila siku na wakati mwingine kuishia kuilalamikia serikali
iliyo madarakani.
“Kwa kuwa nchi yetu
inafuata misingi ya utawala bora na utawala wa sheria, uliojikita katika kutoa
huduma bora kwa wananchi, niliziagiza ofisi za umma mkoani Iringa kutenga siku
maalum ya kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kuitangaza siku hiyo ili
wananchi waifahamu” alisema mheshimiwa Masenza.
Katika
kufanikisha agizo hilo, Mkuu wa Mkoa amezitaka ofisi za umma kuunda kamati kwa
ajili ya kupokea na kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kuyatafutia
ufumbuzi wa kudumu na kutoa mrejesho kwa wananchi walalamikaji.
“Upokeaji na usikilizaji wa kero na malalamiko
ya wananchi uende sambamba na kuorodhesha kero na malalamiko hayo katika
daftari la kudumu likionesha jina la mlalamikaji, aina ya lalamiko, afisa
aliyepokea lalamiko husika, tarehe ya kupokea na kulitatua, mrejesho na maoni”
alisisitiza mheshimiwa Masenza.
Ofisi
ya mkuu wa mkoa wa Iringa imetenga siku ya jumatatu ya kila wiki ya kazi kwa
ajili ya kupokea, kusikiliza na kutatua ufumbuzi wa kero na malalamiko ya
wananchi.
=30=
No comments:
Post a Comment