Thursday, January 26, 2017

KILOLO YATAKIWA KUZIDISHA KASI UJENZI WA MADARASA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wilaya ya Kilolo imetakiwa kuongeza juhudi katika ujenzi wa madarasa na majengo ya utawala ili wanafunzi waweze kusoma vizuri bila kubanana jambo linaloathiri ufanisi katika masomo yao.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipofanya ziara ya kukagua wanafunzi walioripoti shuleni na hali ya miundombinu ya elimu wilayani Kilolo jana.

Masenza alisema “kuna shule za msingi madawati hayajakamilika na vyumba vya madarasa pungufu. Hii maana yake maafisa watendaji wa kata na vijiji hawajatimiza wajibu wao”. Afisa utumishi lazima upitie mipango kazi ya maafisa watendaji wa kata na vijiji ili kujiridhisha kama wameweka katika mipango ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa. Aliongeza kuwa zipo baadhi ya shule za msingi zina upungufu wa miundombinu ya vyoo. Aliutaka uongozi wa wilaya kusimamia ukamilishaji wa miundombinu yote ya elimu ili iwe chachu kwa walimu kufundisha vizuri na watoto kusoma zaidi.

Mkuu wa mkoa huyo aliwataka wana Kilolo kuwa wamoja na kufanya kazi kwa umoja ili kuzitatua changamoto zinazoikabili wilaya hiyo. “Changamoto katika elimu ni nyingi wilayani hapa, umoja wenu ndiyo njia pekee ya kutatua changamoto hizi” alisema Masenza.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya uandikishaji wanafunzi katika shule ya msingi Utengule, mwalimu mkuu Grayson Kwayu alisema kuwa wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza matarajio yalikuwa kuandikisha wanafunzi 76 hadi kufikia tarehe 24/1/2017 jumla la wanafunzi 86 walikuwa wameandikishwa shuleni hapo.

Akiongelea hali ya uandikishaji darasa la awali, mwalimu Kwayu alisema kuwa matarajio yalikuwa kuandikisha watoto 96 kwa darasa la awali, hadi kufikia tarehe 24/1/2017 ni wanafunzi 66 pekee waliokuwa wameandikishwa.

Akiongelea nyumba za walimu, mwalimu mkuu huyo alisema kuwa shule yake inaupungufu wa nyumba za walimu tano. Alisema kuwa mahitaji ya nyumba za walimu ni 14 wakati nyumba zilizopo ni tisa. ”Kamati ya shule kwa kushirikiana na serikali ya kijiji imeandaa mpango kazi kwa ajili ya kujenga maboma matano ya nyumba za walimu kwa kipindi cha mwaka 2017-2020” alisema Kwayu.

Shule ya msingi Utengule ina jumla ya walimu 14, walimu saba wakiwa wa kiume na walimu saba wa kike.
=30=    

WALIMU, TUMIENI VIZURI ZANA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Walimu wa elimu ya awali wa mikoa ya Iringa na Njombe wametakiwa kutumia vizuri mbinu za ufundishaji na kutoa nafasi kubwa kwa mtoto kujifunza.

Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Njombe, Stephen Bange alipokuwa akifunga mafunzo ya walimu wa elimu ya awali yaliyofanyika katika chuo cha ualimu Kleruu mjini Iringa jana.

Bange alisema “mtakapokwenda kufundisha hamna budi kutumia kwa usahihi mbinu za ufundishaji mlizojifunza na kuhakikisha kuwa mnatoa nafasi kubwa kwa mtoto kuweza kujifunza. Mbinu zote zitilie mkazo kwa mtoto kutumia mazingira halisi katika kujifunza. Mtoto apewe muda wa kufanya vitendo na majaribio yanayolingana na umri wake”. Aliongeza kuwa mtoto awezeshwe kutumia vitu halisi katika kujifunza. Mwalimu anapaswa kuandaa mazingira mazuri ya kujifunzia na kuandaa zana zenye mvuto na zinazokuza udadisi. 

Bange aliwataka walimu hao kuwashirikisha walimu ambao hawakushiriki mafunzo hayo, mambo yote waliyojifunza ili nao wawe mahili ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa walivyotumia wakati wa mafunzo. 

Vilevile, aliwataka kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa ufundishaji na ujifunzaji ili kutekeleza mtaala wa elimu ya awali kwa ufanisi. 

Katika taarifa ya mafunzo iliyowasilishwa na Mratibu wa mafunzo, kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, Laurence Kunambi alisema kuwa taasisi ya elimu Tanzania imeboresha mitaala yote ya elimu msingi kutoka elimu ya awali mpaka darasa la sita. Taasisi imeshafanya maandalizi ya kuboresha mtaala wa elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi nne. Aliongeza kuwa TET imekwisha andaa vitabu vya kiada kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza hadi la sita pamoja na ngazi ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne. Aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza TET imeandaa vitabu vya kiada kwa kidato cha tano na sita.

Akiongelea mafunzo juu ya uboreshaji mtaala wa elimu ya awali yamefanyika kwa awamu nne, ambapo awamu ya kwanza yalihusisha wawezeshaji wa kitaifa 22. Awamu ya pili mafunzo yalihusisha wawezeshaji wa mikoa 375. Awamu ya tatu ambayo ndiyo hii inahusu mafunzo ya walimu wa elimu ya awali 16,129 katika vituo 18 nchi nzima.

Alisema kuwa katika mkoa wa Iringa na Njombe, walimu 957 watapatiwa mafunzo katika kituo cha chuo cha Kreluu.

Kunambi alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuwajengea walimu wa elimu ya awali uwezo wa kutekeleza mtaala na muhtasari wa elimu ya awali ulioboreshwa wa mwaka 2016. Malengo mengine aliyataja kuwa ni kukuza uelewa wa dhana ya mtaala na muhtasari wa elimu ya awali na kumuwezesha mwalimu kutumia mtaala na muhtasari na vifaa vyake. 

Mengine ni kumuwezesha mwalimu kujenga uwezo wa kuhusisha kitabu na umahiri husika. Kubaini, kufaragua, kutengeneza na kutumia zana stahiki katika kufundisha na kujifunza na kumuwezesha mwlimu kujenga uwezo wa kufanya maandalizi sahihi ya ufundishaji.
=30=

IRINGA YAONGEZA UFAULU DARASA LA SABA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza ufaulu kwa zaidi ya asilimia tisa kwa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2016.

Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Richard Mfugale alipowasilisha taarifa ya maendeleo ya elimu ya mkoa wa Iringa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa. 

Mfugale alisema “mkoa wa Iringa umepanda ufaulu kwa asilimia 9.62 kutoka asilimia 73.25 (mwaka 2015) hadi asilimia 82.87 (mwaka 2016) na kushika nafasi ya tatu kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara. Mkoa haukuwa na tuhuma za udaanganyifu wa mtihni kwa mwaka 2016”

Alisema kuwa shule za msingi 472, kati ya shule 496 ndizo zilikuwa na watahimiwa waliofanya mtihani. Wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 21,177, kati ya wanafunzi waliosajiliwa 21,270. Wanafunzi 93 hawakufanya mtihani kutokana na sababu za utoro, vifo, ugonjwa, mimba na kuhama. Alizitaja taakwimu hizo kuwa ni utoro (76), vifo (7), ugonjwa (8), mimba (1) na kuhama (1). 

Akiongelea hali ya miundombinu na samani katika shule za msingi, kaimu afisa elimu mkoa alisema “miundombinu na samani ni nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu. Mkoa umeendelea kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu na samani vinapatikana katika shule ili ziweze kutoa elimu bora”. Alisema kuwa upo upungufu wa miundombinu hasa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, maabara, maktaba na majengo ya utawala. 

Aliongeza kuwa mkoa umeendelea kuhamasisha wadau kuchangia madawati ambapo mkoa hauna upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari. “Aidha, upungufu unaweza kujitokeza baada ya kufungua kwa shule za msingi na sekondari kutokana na uandikishaji wa wanafunzi wa awali na msingi na tarehe 15 aprili, 2017 kwa shule za sekondari ambapo zoezi la kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara litamalizika” alisisitiza Mwl Mfugale.
=30=

LAMI YA ST. DOMINIC YAKAMILIKA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imekalimisha ujenzi wa barabara ya St. Dominic kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya shilingi 290,000,000.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mhandisi wa Manispaa ya Iringa, Mhandisi Richard Moshi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kazi za matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2015/2016 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa mjini Iringa.

Mhandisi Moshi alisema kuwa katika mpango wa mwaka, upatikanaji wa huduma za miundombinu na mawasiliano kuboreshwa, ilipangwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami barabara ya St. Dominic na kipande cha Ilala km 0.76 kwa kiwango cha lami. Alisema kuwa katika utekelezaji wa ujenzi huo, fedha iliyotengwa ni shilingi 348,614,279.40 wakati fedha iliyotumika ni shilingi 290,521,317.91 na mradi umekamilika na upo katika muda wa matazamio.   

Mhandisi Moshi alieleza ujenzi wa mifereji eneo la Mawelewele kata ya Mwangata km 2.3 na kuweka changarawe km 1.0 mtaa wa Kibarabara. “Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 85 kwa gharama ya shilingi 290,694,241” alisema Mhandisi Moshi.

Akiongelea matengenezo ya muda maalum ya barabara ya Makanyagio 1.5 km, shughuli iliyofanyika ni kuchimba mtaro na matengenezo hayo yamefikia asilimia 15. Aidha, fedha, zilizotengwa kwa matengenezo hayo ni shilingi 84,700,518.

Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ina mtandao wa barabara zenye urefu wa km 525.969, kati ya barabara hizo, km 50.165 ni barabara kuu na barabara za Mkoa ambazo zinahudumiwa na Wakala wa barabara nchini (TANROADS) kwa matengenezo. Km 475.804 ni barabara zilizo chini ya mamlaka ya Manispaa na matengenezo yake hufanywa na Halmashauri ya Manispaa. Kati ya km 19.483 ni za lami, km 125.439 ni za changarawe na km 341.057 ni za udongo.
=30= 



SHILINGI 15,614.372 MILIONI KUTENGENEZA BARABARA IRINGA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umepangiwa shilingi 15,614.372 milioni kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara na miradi ya maendeleo hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2016 katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Mkwawa, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Daniel Kindole, alisema “jumla ya shilingi 15,614.372 milioni zimepangwa kutumika katika miradi mbalimbali ya matengenezo na ukarabati wa barabara mkoani Iringa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Mhandisi Kindole alisema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi 13,896.372 zinatoka mfuko wa barabara na shilingi 1,718.000 zinatoka mfuko wa maendeleo. 

Akielezea mchanganuo wa mpango wa matengenezo kwa fedha za mfuko wa barabaara, Meneja wa TANROADS Mkoa alisema kuwa barabara kuu zimetengewa shilingi 4,555.751 milioni kwa ajili ya matengenezo maalumu ya madaraja matano (shilingi 188.800 milioni), matengenezo ya kinga ya madaraja 140 (shilingi 140.000 milioni), matengenezo maalum kwa barabara za changarawe/ udongo km 16.6 (shulingi 502.587 milioni), matengenezo maalum barabara za lami km 3.8 (shilingi 1,683.853 milioni). Matengenezo mengine aliyataja kuw ni matengenezo ya kawaida baraabara za changarawe/ udongo km 66.8 (shilingi 422.192 milioni) na matengenezo ya kawaida barabara ya lami km 317.5 (shilingi 1,618.319 milioni).

Akiongelea barabara za mikoa, Mhandisi Kindole alisema kuwa matengenezo ya kawaida baraabara za lami, km 26.7 (shilingi 171.240 milioni), matengenezo ya kawaida barabara za chanagarawe/ udongo km 709.7 (shilingi 3,161.640 milioni), matengenezo maalum barabara za lami km 3.5 (shilingi 1,540.980). Matengenezo mengine ni matengenezo maalum barabara za changarawe/udongo km 158.3 (shilingi 3,843.528), matengenezo ya kuboresha barabara za changarawe km 18.3 (shilingi 354.833 milioni), matengenezo ya kinga ya madaraja 65 (shilingi 115.000 milioni) na matengenezo maalum ya madaraja 7 (shilingi 153.400 milioni).

Kuhusu mpango wa ukarabati wa barabara –miradi ya maendeleo, Meneja huyo alisema kuwa mpango huo utahusisha ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara mbili km 0.7 kwa shilingi 362.000 milioni. Mpango mwingine ni ujenzi wa daraja (Lukosi II) shilingi 100.000 milioni, ukarabati wa kiwango cha lami km 0.3 kwa shilingi 250.000 milioni na ukarabati wa kiwango cha changarawe kwa barabara nane kwa jumla ya km 52 shilingi 1006.000 milioni.
=30=