Thursday, January 26, 2017

IRINGA YAONGEZA UFAULU DARASA LA SABA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza ufaulu kwa zaidi ya asilimia tisa kwa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2016.

Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Richard Mfugale alipowasilisha taarifa ya maendeleo ya elimu ya mkoa wa Iringa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa. 

Mfugale alisema “mkoa wa Iringa umepanda ufaulu kwa asilimia 9.62 kutoka asilimia 73.25 (mwaka 2015) hadi asilimia 82.87 (mwaka 2016) na kushika nafasi ya tatu kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara. Mkoa haukuwa na tuhuma za udaanganyifu wa mtihni kwa mwaka 2016”

Alisema kuwa shule za msingi 472, kati ya shule 496 ndizo zilikuwa na watahimiwa waliofanya mtihani. Wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 21,177, kati ya wanafunzi waliosajiliwa 21,270. Wanafunzi 93 hawakufanya mtihani kutokana na sababu za utoro, vifo, ugonjwa, mimba na kuhama. Alizitaja taakwimu hizo kuwa ni utoro (76), vifo (7), ugonjwa (8), mimba (1) na kuhama (1). 

Akiongelea hali ya miundombinu na samani katika shule za msingi, kaimu afisa elimu mkoa alisema “miundombinu na samani ni nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu. Mkoa umeendelea kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu na samani vinapatikana katika shule ili ziweze kutoa elimu bora”. Alisema kuwa upo upungufu wa miundombinu hasa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, maabara, maktaba na majengo ya utawala. 

Aliongeza kuwa mkoa umeendelea kuhamasisha wadau kuchangia madawati ambapo mkoa hauna upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari. “Aidha, upungufu unaweza kujitokeza baada ya kufungua kwa shule za msingi na sekondari kutokana na uandikishaji wa wanafunzi wa awali na msingi na tarehe 15 aprili, 2017 kwa shule za sekondari ambapo zoezi la kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara litamalizika” alisisitiza Mwl Mfugale.
=30=

No comments:

Post a Comment