Thursday, January 26, 2017

KILOLO YATAKIWA KUZIDISHA KASI UJENZI WA MADARASA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wilaya ya Kilolo imetakiwa kuongeza juhudi katika ujenzi wa madarasa na majengo ya utawala ili wanafunzi waweze kusoma vizuri bila kubanana jambo linaloathiri ufanisi katika masomo yao.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipofanya ziara ya kukagua wanafunzi walioripoti shuleni na hali ya miundombinu ya elimu wilayani Kilolo jana.

Masenza alisema “kuna shule za msingi madawati hayajakamilika na vyumba vya madarasa pungufu. Hii maana yake maafisa watendaji wa kata na vijiji hawajatimiza wajibu wao”. Afisa utumishi lazima upitie mipango kazi ya maafisa watendaji wa kata na vijiji ili kujiridhisha kama wameweka katika mipango ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa. Aliongeza kuwa zipo baadhi ya shule za msingi zina upungufu wa miundombinu ya vyoo. Aliutaka uongozi wa wilaya kusimamia ukamilishaji wa miundombinu yote ya elimu ili iwe chachu kwa walimu kufundisha vizuri na watoto kusoma zaidi.

Mkuu wa mkoa huyo aliwataka wana Kilolo kuwa wamoja na kufanya kazi kwa umoja ili kuzitatua changamoto zinazoikabili wilaya hiyo. “Changamoto katika elimu ni nyingi wilayani hapa, umoja wenu ndiyo njia pekee ya kutatua changamoto hizi” alisema Masenza.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya uandikishaji wanafunzi katika shule ya msingi Utengule, mwalimu mkuu Grayson Kwayu alisema kuwa wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza matarajio yalikuwa kuandikisha wanafunzi 76 hadi kufikia tarehe 24/1/2017 jumla la wanafunzi 86 walikuwa wameandikishwa shuleni hapo.

Akiongelea hali ya uandikishaji darasa la awali, mwalimu Kwayu alisema kuwa matarajio yalikuwa kuandikisha watoto 96 kwa darasa la awali, hadi kufikia tarehe 24/1/2017 ni wanafunzi 66 pekee waliokuwa wameandikishwa.

Akiongelea nyumba za walimu, mwalimu mkuu huyo alisema kuwa shule yake inaupungufu wa nyumba za walimu tano. Alisema kuwa mahitaji ya nyumba za walimu ni 14 wakati nyumba zilizopo ni tisa. ”Kamati ya shule kwa kushirikiana na serikali ya kijiji imeandaa mpango kazi kwa ajili ya kujenga maboma matano ya nyumba za walimu kwa kipindi cha mwaka 2017-2020” alisema Kwayu.

Shule ya msingi Utengule ina jumla ya walimu 14, walimu saba wakiwa wa kiume na walimu saba wa kike.
=30=    

No comments:

Post a Comment