Thursday, January 26, 2017

HALMASHAURI ZATAKIWA KUINGIZA WATEJA KWENYE MFUMO WA MALIPO YA KODI



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri za mkoa wa Iringa zimetakiwa kuingiza wateja wote wa ardhi katika mfumo wa ukusanyaji mapato ya ardhi wa kieletroniki ili serikali iweze kupata mapato yake na kutoa huduza za kijamii.

Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dr. Angelina Mabula mjini Mafinga alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa ya kukagua mifumo wa ukusanyaji mapayo ya ardhi mkoani Iringa.

Dr. Mabula alisema “Halmashauri zote zimefungiwa mfumo wa ukusanyaji mapato, ila takwimu zao hazijakaa sawa. Halmashauri hazijaweka utaratibu mzuri wa kuweka kumbukumbu. Hivyo, naagiza kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2017, Halmashauri zote lazima wateja wake wote wawe wameingizwa katika mfuko wa ukusanyaji mapato ya ardhi”. 

Alisema kuwa utaratibu wa kutoingiza wateja wote katika mfumo, unaikosesha serikali mapato kwa sababu Halmashauri zinashindwa kuwatambua wateja wote wanaodaiwa. “Kutokana na kushindwa kuwafahamu wateja wote, hata malengo yanayokadiliwa katika bajeti yanakuwa chini sana ikilinganishwa na uhalisia” alisema Dr. Mabula. Aliongeza kuwa, Afisa Ardhi yeyote mteule, atakayeshindwa kufikia malengo ya kuingiza wateja wote katika mfuko wa ukusanayaji mapato atatenguliwa nafasi yake na nafasi hiyo kupewa mtu mwingine.

Naibu Waziri alizishauri Halmashauri kuweka utaratibu wa kutoa notisi za kuwakumbusha wateja wadaiwa wa kodi ya ardhi mara kwa mara ili kuwakumbusha kulipa tofauti na utaratibu uliopo sasa.
Alisema kuwa changamoto ya mfuko kushindwa kuwapata wateja wote wadaiwa kwa mara moja imechukuliwa na wizara yake na itaenda kufaanyiwa kazi. Vilevile, alizitaka Halmashauri kukusanya madeni yote ya ardhi kwa wateja ili fedha hizo ziweze kutumika katika utaratibu wa serikali.

Akiongelea ngogoro wa mpaka kati ya wilaya za Iringa na Kilolo, katika vijiji vya Ilole na Ilambilole, Dr. Mabula alisemaa kuwa vijiji vyote vina GN jambo ambalo si la kawaida. Aliagiza kuwa GN hizo zipitiwe upya ili kupatiwa suluhisho. Aliwataka wakuu wa wilaya kuendelea kutatua migogoro iliyopo katika maeneo yao kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili kusikiliza na kutatua kero zao.

Akiongelea sababu za migogoro ya ardhi, Naibu Waziri alisema kuwa migogoro mingi ya ardhi inachangiwa na kutokuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi kati ya wakuma na wafugaji. “Nazitaka Halmashauri kutambua idadi ya wafugaji na mifugo waliyonayo ili kupanga matumizi bora ya ardhi” aliagiza Naibu Waziri. Pia aliwataka wakuu wa wilaya kushiriki katika mikutano ya ugawaji ardhi ili kusimamia taratibu zilizopo kufuatwa.     
=30=

No comments:

Post a Comment