Thursday, January 26, 2017

IRINGA KUSIMAMIA VIKUNDI VYA WAFUGAJI KUONGEZA THAMANI YA MAZAO



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali mkoani Iringa imeendelea kuhamasisha uundaji wa vikundi vya wafugaji ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.

Kauli iyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya maendeleo ya mkoa wa Iringa kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyefanya ziara fupi mkoani Iringa jana.

Masenza alisema “Halmashauri za mkoa wa Iringa zimeweza kuendelea kuhamasisha uundwaji wa vikundi vya wafugaji ili kuboresha ufugaji na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo. Kwa sasa mkoa una vyama vitatu vya ushirika vya wafugaji. Vyama hivi vinasaidia wanachama kuwa na vituo maalum vya kukusanya maziwa na kuuza kiwandani pamoja na kusaidia wanachama kwa pamoja kupata elimu ya ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wa maziwa”.

Aliongeza kuwa idara ya Magereza mkoani hapa inaendelea na mradi wa ufugaji ng’ombe wa maziwa na serikali imeunganisha idara hiyo na kampuni ya ASAS ili kuweza kuzalisha ng’ombe wa maziwa kwa njia ya kisasa zaidi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 23,268,437 mwaka 2015 hadi lita 29,366,559 mwaka 2016. “Uzalishaji huu bado hautoshi, lengo la mkoa ni kufikia uzalishaji wa lita 40,000,000 ifikapo Disemba, 2017” alisema Masenza. 

Mkoa umekuwa ukitoa elimu kwa wafugaji ya namna bora ya kuchanja na kuogesha mifugo yao kwa wakati. Elimu imesaidia kujikinga na magonjwa hatari kama ndigana kali na baridi, ugonjwa wa kuoza miguu na midomo na ugonjwa wa mapafu.
=30=

No comments:

Post a Comment