Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Walimu
wa elimu ya awali wa mikoa ya Iringa na Njombe wametakiwa kutumia vizuri mbinu
za ufundishaji na kutoa nafasi kubwa kwa mtoto kujifunza.
Kauli
hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Njombe, Stephen Bange
alipokuwa akifunga mafunzo ya walimu wa elimu ya awali yaliyofanyika katika
chuo cha ualimu Kleruu mjini Iringa jana.
Bange
alisema “mtakapokwenda kufundisha hamna
budi kutumia kwa usahihi mbinu za ufundishaji mlizojifunza na kuhakikisha kuwa
mnatoa nafasi kubwa kwa mtoto kuweza kujifunza. Mbinu zote zitilie mkazo kwa
mtoto kutumia mazingira halisi katika kujifunza. Mtoto apewe muda wa kufanya
vitendo na majaribio yanayolingana na umri wake”. Aliongeza kuwa mtoto
awezeshwe kutumia vitu halisi katika kujifunza. Mwalimu anapaswa kuandaa
mazingira mazuri ya kujifunzia na kuandaa zana zenye mvuto na zinazokuza
udadisi.
Bange
aliwataka walimu hao kuwashirikisha walimu ambao hawakushiriki mafunzo hayo,
mambo yote waliyojifunza ili nao wawe mahili ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa
walivyotumia wakati wa mafunzo.
Vilevile, aliwataka kutatua changamoto
zinazojitokeza wakati wa ufundishaji na ujifunzaji ili kutekeleza mtaala wa
elimu ya awali kwa ufanisi.
Katika
taarifa ya mafunzo iliyowasilishwa na Mratibu wa mafunzo, kutoka Taasisi ya
Elimu Tanzania, Laurence Kunambi alisema kuwa taasisi ya elimu Tanzania
imeboresha mitaala yote ya elimu msingi kutoka elimu ya awali mpaka darasa la
sita. Taasisi imeshafanya maandalizi ya kuboresha mtaala wa elimu ya sekondari
kidato cha kwanza hadi nne. Aliongeza kuwa TET imekwisha andaa vitabu vya kiada
kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza hadi la sita pamoja na ngazi ya
sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne. Aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza TET
imeandaa vitabu vya kiada kwa kidato cha tano na sita.
Akiongelea
mafunzo juu ya uboreshaji mtaala wa elimu ya awali yamefanyika kwa awamu nne,
ambapo awamu ya kwanza yalihusisha wawezeshaji wa kitaifa 22. Awamu ya pili
mafunzo yalihusisha wawezeshaji wa mikoa 375. Awamu ya tatu ambayo ndiyo hii
inahusu mafunzo ya walimu wa elimu ya awali 16,129 katika vituo 18 nchi nzima.
Alisema
kuwa katika mkoa wa Iringa na Njombe, walimu 957 watapatiwa mafunzo katika
kituo cha chuo cha Kreluu.
Kunambi
alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuwajengea walimu wa elimu ya awali uwezo
wa kutekeleza mtaala na muhtasari wa elimu ya awali ulioboreshwa wa mwaka 2016.
Malengo mengine aliyataja kuwa ni kukuza uelewa wa dhana ya mtaala na muhtasari
wa elimu ya awali na kumuwezesha mwalimu kutumia mtaala na muhtasari na vifaa
vyake.
Mengine
ni kumuwezesha mwalimu kujenga uwezo wa kuhusisha kitabu na umahiri husika.
Kubaini, kufaragua, kutengeneza na kutumia zana stahiki katika kufundisha na
kujifunza na kumuwezesha mwlimu kujenga uwezo wa kufanya maandalizi sahihi ya
ufundishaji.
=30=
No comments:
Post a Comment