Thursday, January 26, 2017

WATU WAPOTEZA HAKI KWA KUTOKUJUA KUSOMA NA KUANDIKA



Na Mwandishi Maalum Iringa
Serikali imesema kuwa watu wengi wamekuwa wakipoteza haki zao za msingi kutokana na kutokujua kusoma na kuandika nchini. 

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akiongea na wananchi wa kata ya Ibumu wilayani Kilolo jana.

Mhandisi Manyanya alisema “ndugu zangu, kutokujua kusoma na kuandika kumewafanya wananchi wengi kupoteza haki zao katika kupiga kura. Wapo watu wamedanganywa na kushindwa kufanya maamuzi sahihi wakati wa upigaji kura. Watu wengine kwa kutokujua kusoma na kuandika wameibiwa katika kufanya miamala ya fedha. 

Aidha, siri za watu zimewekwa hadharani na watu ambao waliwaamini. Hivyo, kujua kusoma na kuandika ni jambo la msingi sana”.

Aidha, aliutaka uongozi wa wilaya ya Kilolo kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapelekwa ili kuondoa tatizo la ucheleweshaji watoto kuanza shule. Alisema kuwa kuwachelewesha watoto kuanza shule kunapelekea baadhi yao kulazimika kuanza kujifunza elimu kupitia mfumo usio rasmi na Memkwa. 

Kupitia mfumo usio rasmi baadhi yao wamekuwa wakiishia njiani kutokana na kukata tamaa. “Katika hili la kupeleka mtoto shule, mzazi au mlezi yeyote atakayekaidi achukuliwe hatua. Wazazi na walezi wameacha kupeleka watoto wao shule, kutwa wanawapeleka mkoani Dar es Salaam kufanya kazi za ndani. Kama ni kufanya kazi waende baada ya kumaliza shule. Watoto wadogo hata maana ya kazi na mshahara hawajafahamu” alisisitiza Mhandisi Manyanya.

Naibu Waziri alisema kuwa suala la kusoma na kuandika katika jamii ni la muhimu sana na halitakiwi kuonewa aibu. “Tusilionee aibu suala hili. Wabunge kama kweli tunawapenda wananchi wetu, lazima tuwahimize kusoma na kuandika. Jambo hili litafanya tuache kumbukumbu na historia nzuri kwenye majimbo yetu” alisisitiza Mhandisi Manyanya. Katika kuhakikisha jamii inajua kusoma na kuandika, aliagiza kuanzishwa kwa madarasa ya watu wazima katika maeneo mbalimbali ili watu waliokosa fursa hiyo waweze kuipata nje ya mfumo rasmi na elimu hiyo ipewe uzito mkubwa.

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Iringa una kiwango cha asilimia 18 cha watu wasiojua kusoma na kuandika. 
=30=    

            

No comments:

Post a Comment