Thursday, January 26, 2017

MUFINDI DC YAANDAA HATI 500



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya wilaya ya Mufindi imefanikiwa kuandaa hati zaidi ya 500 kwa mujibu wa sheria.

Akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Mufindi kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017, Wilaya ya Mufindi inaendelea kutekeleza kazi mbalimbali ikiwemo uandaaji wa hati chini ya sheria namba 4 ya mwaka 1999. “Jumla ya hati 533 (Mji Mafinga 474 na Wilaya ya Mufindi 59) zimeandaliwa na hati chini ya sheria namba 5 ya mwaka 1999 zimeandaliwa jumla ya hati 512 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi” alisema William.

Akiongelea ukusanyaji wa mapato ya ardhi, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi alisema kuwa katika kutekeleza ukusanyaji wa mapato ya ardhi, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na mwaka 2016/2017 makusanyo ya kodi za ardhi Wilaya ya Mufindi yalikuwa 1053427600. Aliongeza kuwa katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga kodi ilikuwa shilingi 457,430,426 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi shilingi 595,997,174.

Akiongelea Mipango miji na vijiji, William alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017, wilaya yake iliandaa michoro ya mipango miji 17 (michoro 12 katika Mji wa Mafinga na michoro mitano katika Halmashauri ya wilaya ya Mufindi). Aliongeza kuwa vijiji 47 vina mipango ya matumizi bora ya ardhi wilayani hapo. Alisema kuwa jitihada zinafanywa na wilaya yake kuhakikisha vijiji vilivyobaki kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali vinakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.  

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya yake katika kipindi cha mwaka 2015/2016 na 2016/2017 ilifanikiwa kupima viwanja 782 (Halmashauri ya Mji wa Mafinga 749 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi 33).

Kwa upande wa uthamini wa mali, alisema kuwa wilaya yake inaendelea na zoezi la uthamini wa nyumba za wananchi ambapo nyumba 710 zimekwisha thaminiwa. Aliongeza kuwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga ilikamilisha zoezi la uthamini na taarifa ilishawasilishwa kwa mthamini mkuu wa serikali kwa ajili ya kupata idhini.
=30=
 

No comments:

Post a Comment