Thursday, January 26, 2017

KUU IRINGA YAPONGEZWA KUDUMISHA AMANI



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Iringa imepongezwa kwa kusimamia amani na usalama mkoani hapa.

Pongezi hizo zilitolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akiongea na watumishi wa shamba la mifugo la Asas na wananchi wa Iringa kwa ujumla alipofanya ziara fupi ya kukagua shamba hilo lililopo Igingilanyi wilayani Iringa.

Majaliwa alisema “leo napita kwenye shamba hili ila ziarani nitapita kiwanadani. Muhimu zaidi ni ulinzi na usalama. Pongezi kwa kamati ya ulinzi na usalama mkoa kusimamia amani na usalama. Endeleeni kuhakiki uingiaji holela wa raia wa kigeni. Uhamiaji imarisheni ulinzi katika mipaka. Tuendelee kuilinda nchi na mipaka yake”

Akiongelea matumizi ya ardhi, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri zote kusimamia matumizi bora ya ardhi. Alizitaka Halmashauri kuhakikisha kila mwenye nyumba anapewa hati. Aliziasa Halmashauari kuwa makini na utoaji wa hati mbili kwa kiwanja kimoja. “Halmashauri punguzeni migogoro hii. Wote tunaowagawia mashamba makubwa wapewe hati za umiliki kwa miaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria” alisisitiza Majaliwa.  

Waziri Mkuu alisema kuwa wengi wenye mifugo, hawaifugi bali wanaichunga. Alisema mifugo ni mingi ila haijaleta tija kwa wenye mifugo. Alizitaka Sekretarieti za mikoa kutoa elimu kwa wafugaji ili wafuge kisasa. Katika kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima, Waziri Mkuu aliagiza mifugo yote nchini kuwekwa alama ya utambulisho wa eneo husika. 

Kuhusu ufugaji katika shamba la mifugo la Asas, Majaliwa alisema “tunayo sababu ya kuendelea kumuunga mkono Asas kwa sababu anafuga kitaalam, katika mashamba yake ameajili watu wengi. Asas pia ananunua bidhaa za wafugaji wanaomzunguka. Endelea kupanua shamba, na serikali itakuunga mkono. Wewe unaunga mkono moja kwa moja azma ya serikali ya awamu ya tano na kuwa nchi ya viwanda”.

Waziri Mkuu alifanya ziara fupi katika shamba la mifugo mkoani Iringa wakati akiwa njiani kuelekea ziarani mkoani Njombe.
=30=

No comments:

Post a Comment