Wednesday, January 17, 2018

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA TIMU KUTOKA CHUO CHA TAIFA CHA ULINZI MKOANI IRINGA















PATO LA MKOA WA IRINGA LIMEONGEZEKA HADI TRILIONI 5.1



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza pato lake hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni tano mwaka 2016 na kuufanya kuwa Mkoa wa tano kwa kigezo cha GDP kitaifa.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania waliofanya ziara ya mafunzo ya siku tano mkoani Iringa katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza (kulia) na Katibu Tawala Mkoa Wamoja Ayubu
Masenza alisema pato la Mkoa wa Iringa (GDP) limeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi trilioni 5.10 Mwaka 2016, wakati pato la mkazi [Per Capita GDP) mwaka 2010 lilikuwa shilingi 1,330,118 ambalo limeongezeka hadi kufikia shilingi 2,982,569 mwaka 2016”. Aliongeza kuwa takwimu hizo za (GDP) kwa mwaka 2016, Mkoa wa Iringa umekuwa ni Mkoa wa tano kwa ngazi ya GDP kitaifa na Mkoa wa tatu kwa pato la mkazi ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam na Mbeya. Aliongeza kuwa pato la Mkoa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na mashamba makubwa ya chai, viwanda vya chai, misitu, viwanda vya mbao na tumbaku.

Akiongelea shughuli za kiuchumi, mkuu wa Mkoa alizitaja kuwa ni kilimo, ufugaji, upasuaji mbao, uvuvi, biashara, ajira za ofisini na viwandani. “Asilimia 75 ya wakazi wa Mkoa huu hujishughulisha zaidi na Kilimo pamoja na ufugaji. Mazao ya kilimo yanayolimwa katika Mkoa huu ni mahindi, maharage, mpunga, ngano, viazi, pareto, chai, matunda, alizeti, karanga, ufuta, nyanya, vitunguu, tumbaku, soya na mtama” alisema Masenza.

Nae kiongozi wa msafara wa wajumbe kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Kapten Msafiri Hamisi alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Mkoa katika kuwahudumia wananchi. Aidha, alishukuru mapokezi waliyopewa na uongozi wa Mkoa na kuomba ushirikiano huo uwe undelevu.

Akitoa neno la shukrani, kiongozi wa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi ya Mkoa na kazi zinazofanywa na Mkoa za kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo. Aidha, aliahidi wanafunzi wa chuo cha Taifa cha ulinzi kuwa balozi wazuri kwa mkoa wa Iringa.

Kwa matokeo ya Sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watu 941,238 kati ya hao wanaume walikuwa 452,052 na wanawake 489,186 na wastani wa ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka ni asilimia 1.1. Makadirio ya idadi ya watu kwa mwaka 2017 ni watu 1,000,040; wanaume wakiwa 480,293 na wanawake 519,747.
=30= 

KILIMO KINACHANGIA ASILIMIA 85 YA PATO LA MKOA IRINGA




Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Sekta ya kilimo inachangia katika usalama wa chakula na utoaji ajira na uchumi wa Mkoa wa Iringa.


Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa waliofanya ziara ya mafunzo ya siku tano mkoani Iringa katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa jana.

Masenza alisema “sekta ya kilimo katika Mkoa ni muhimili mkuu wa uchumi na inachangia katika usalama wa chakula na utoaji wa ajira. Sekta hii inachangia takribani asilimia 85 ya pato la Mkoa kwa mujibu wa wasifu wa kiuchumi na Kijamii, mwaka 2013”. Alisema kuwa lengo la Mkoa ni kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na chakula cha kutosha, wanaongeza kipato na uhakika wa upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda.


Akiongelea sekta ya mifugo na uvuvi, mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema kuwa Mkoa wa Iringa una mashamba makubwa ya mifugo 20 yanayomilikiwa na serikali na watu binafsi. Alisema kuwa mashamba hayo huzalisha maziwa, mitamba na madume bora.
Mkoa wa Iringa hadi kufikia Juni, 2017 ulikuwa na jumla ya ng’ombe 330,372, mbuzi 160,227, kondoo 62,475, nguruwe 109,131 na kuku wapatao 1,341,718 na eneo linalotumika kwa malisho ni jumla ya hekta 209,003” alisema mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wa uvuvi, alisema kuwa Mkoa una mabwawa madogo 1,893 yaliyochimbwa yanayotumiwa kwa shughuli za uvuvi. Alisema kuwa Mkoa una wavuvi 5,807 ambao hufanya shughuli za uvuvi kama mtu mmoja mmoja na katika vikundi.

Mavuno ya samaki yamekuwa yakiongezeka kutoka Tani 913.50 mwaka 2011/2012 hadi kufikia Tani 1,186.99 mwaka 2014/15.

Akitoa neno la shukrani, kiongozi wa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi ya Mkoa na kazi zinazofanywa na Mkoa za kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo. Aidha, aliahidi wanafunzi wa chuo cha Taifa cha ulinzi kuwa balozi wazuri kwa mkoa wa Iringa.

Kwa matokeo ya Sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watu 941,238 kati ya hao wanaume walikuwa 452,052 na wanawake 489,186 na wastani wa ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka ni asilimia 1.1. Makadirio ya idadi ya watu kwa mwaka 2017 ni watu 1,000,040; wanaume wakiwa 480,293 na wanawake 519,747.
=30=

IRINGA NA MPANGO WA KUBORESHA UTALII



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Mkoa wa Iringa umeandaa mpango wa kuboresha maonesho ya utalii karibu kusini ili kuweza kuwavutia watalii wengi kutembelea vivutio vya utalii na kufurahia mandhari iliyopo katika vivutio hivyo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi waliotembelea Mkoa wa Iringa kwa ziara ya mafunzo.
 
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa na timu kutoka chuo cha Taifa cha Ulinzi
Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa ni kitovu cha utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini. Maonesho ya utalii karibu kusini yanatumika kukuza sekta ya utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini. “Maonesho ya utalii karibu Kusini yanatumika kama mkakati maalum wa kufungua sekta ya utalii kwa ukanda wa Kusini ambao umejaa fursa na vivutio vya kipee katika utalii.

Alitolea mfano maporomoko ya maji ya Kihansi ambapo wanapatikana vyura wa kipekee wanaozaa tofauti na vyura wengine wanaotaga mayai.

Mkoa wa Iringa ukiwa mratibu umeandaa mipango ya kuboresha maonesho haya kwa kutenga eneo la Kihesa Kilolo kama eneo maalum kwa ajili ya maonesho ya utalii karibu kusini. Eneo hili litatumiwa na wadau wa utalii na wadau wa maendeleo kujenga miundombinu kwa ajili ya kuonesha huduma na bidhaa za sekta ya utalii” alisema Masenza.

Akitoa neno la shukrani, kiongozi wa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi ya Mkoa na kazi zinazofanywa na Mkoa za kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo. Aidha, aliahidi wanafunzi wa chuo cha Taifa cha ulinzi kuwa balozi wazuri kwa mkoa wa Iringa.

Mkoa wa Iringa ulifanya maonesho ya kuendeleza utalii ya karibu Kusini kwa miaka miwili mfululizo (mwaka 2016 na 2017) kwa kushirikisha mikoa ya nyanda za juu kusini ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Rukwa na Katavi.
=30=