Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Ushirikishaji wananchi na makundi
mengine katika jamii ni njia rahisi ya kuleta tija katika utekelezaji wa Ilani
ya CCM na miradi ya maendeleo mkoani Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya
Mufindi, Mboni Mhita katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Iringa.
Mhe. Mboni Mhita (kulia) walio kaa na Mhe. Amina Masenza (kushoto). Waliosimama ni Maafisa waandamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa |
Masenza amesema kuwa katika
kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na miradi yote ya maendeleo
katika Wilaya na Mkoa dhana ya ushirikishaji wananchi na wadau wengine ni
muhimu sana katika kuleta tija ya kazi. Amesema wananchi na makundi mengine
yanaposhirikishwa uelewa wa pamoja unakuwepo na kufanya utekelezaji wake kuwa
ni jukumu la jamii nzima. Amesema kuwa mara nyingi mtafaruku na wananchi
unatokea pale ambapo ushirikishwaji unakuwa mdogo au hakuna kabisa.
Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya
kusoma kwa umakini nakala ya wajibu wa Mkuu wa Wilaya na kuuelewa kwa sababu
ndiyo muongozo katika utendaji kazi wa Mkuu wa Wilaya. Amesema kuwa hakuna
jambo lisilowezekana na kumtaka kutumia vizuri vyombo vya usalama na wataalamu
waliopo katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, amemtaka kufanya kazi bega kwa bega na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi ili kazi yake iwe nyepesi. Amesema
kuwa Kamati hiyo inawajibu wa kumshauri na kumsaidia katika kutekeleza majukumu
katika Wilaya ya Mufindi.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa wananchi wote
wanamatumaini na Wakuu wa Wilaya katika kutatua matatizo yao. “Wewe ni lulu,
wananchi wote wataangaika sehemu zote watakazokwenda lakini wakifika kwako
watasema hapa tumefika na hapa ndiyo mwisho. Unamwambia mwananchi nenda
mahakamani hataki, nenda polisi hataki nenda kwa Mkurugenzi hataki anajua wewe
ndiye utaweza kumsimamia na wewe peke yako ndiye unaweza.” Alisisitiza Masenza.
Amesema kuwa wananchi wengi
wanamatumaini sana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa sababu wanamajibu
ya papo kwa papo kwa matatizo ya wananchi kwa vile vyombo walivyonavyo
vinawafanya kuwa na majibu.
Akitoa shukrani zake, Mkuu wa Wilaya
ya Mufindi, Mboni Mhita amemshukuru Mhe. Rais kwa imani aliyonayo kwake na
kumteua katika nafasi hiyo. Aidha, ameomba ushirikiano na ushauri kadri
inavyowezekana ili kazi yake iwe rahisi. Amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kumpatia
nasaha na vitendea kazi. “Mbali na vitabu ambavyo umenipa vya Ilani pamoja na Katiba,
maneno yako yamekuwa na uzito sana naomba nikuahidi kwamba nitayazingatia na
pindi nitakapoona kwamba nimekwama au nahitaji ushauri basi sitasita kuja kwako
kuomba ushauri.” Alisisitiza Mboni.
Tukio hilo la kuapishwa kwa Mkuu wa
Wilaya ya Mufindi limeshuhudiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, familia
ya Mboni, watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Mufindi, waandishi wa
habari na wananchi kwa ujumla.
=30=