Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Uongozi wa Mkoa wa Iringa umepongezwa kwa
mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya elimu kwa kuongeza kiwango cha
ufaulu.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda alipokuwa akifanya
majumuisho ya ziara yake ya Mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Mhe. Pinda amesema “napongeza uongozi wa
Mkoa na Wilaya zote kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya
elimu.” Amesema Mkoa umefanya vizuri katika elimu ya msingi na sekondari kwa
kuongeza ufaulu wa wanafunzi. Amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Mkoa kuhusu
sekta ya elimu, ufaulu wa mtihani wa darasa la saba mwaka 2014 ulikuwa asilimia
68.5 na ufaulu wa kidato cha nne ulikuwa asilimia 65.2.
Akiongelea ufaulu wa kidato cha sita mwaka
2013, Waziri Mkuu amesema kuwa Mkoa ulifanya vizuri na katika matokeo ya kidato
hicho, asilimia 99 ya watahiniwa wote walifaulu. Amesema katika matokeo hayo,
shule ya sekondari Igowole ambayo ni shule ya Kata Wilayani Mufindi iliongoza
kitaifa. Aidha, shule ya sekondari Kawawa pia katika Wilaya ya Mufindi ilikuwa
katika 10 bora kitaifa. Kutokana na mafanikio hayo mazuri, ameutaka uongozi wa
Mkoa kutokurudi nyuma.
Akiongelea agizo la Mhe. Rais la ujenzi wa
Maabara za Sayansi, Mhe. Pinda amewatia moyo viongozi wa Mkoa wa Iringa ili
waendelee na jitihada ya kukamilisha agizo hilo la Mhe. Rais katika kipindi
kilichoongezwa hadi kufikia mwezi Juni, 2015. Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa
nchini kufuatilia ujenzi wa Maabara hizo za Sayansi nchini. Amesema “wito wangu
ni kwa Wakuu wa Mikoa nchini kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa
Maabara hizo za Sayansi ili Wilaya ziweze kufikia malengo yao kabla ya mwezi
Juni 2015.”
Wakati huohuo, amewataka Wakurugenzi wa
Halmashauri nchini kujenga Maabara mpya na za kisasa zinazoendana na mazingira
ya sasa. Amekosoa hatua ya baadhi ya Halmashauri kukarabati Maabara za zamani
zenye majengo yaliyochakaa na kuwakumbusha kuwa lengo la serikali ni kujenga Maabara
mpya za kisasa zitakazodumu.
Mkoa wa Iringa umefikia asilimia 34 ya ujenzi wa Maabara ambayo ni
sawa na Maabara 108 kati ya mahitaji ya Maabara 318. Maabara 210 zipo katika hatua
mbalimbali za umaliziaji.
=30=
No comments:
Post a Comment