Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umepiga
hatua katika kuongeza pato la mwananchi kufikia shilingi 1,660,532 mwaka 2013.
Kauli hiyo imetolewa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku
sita Mkoani Iringa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi.
Mheshimiwa Pinda amesema
kuwa pato la mwananchi wa Mkoa wa Iringa linakua vizuri, mwaka 2006 pato la
mwananchi mmoja mmoja lililuwa shilingi 589,607 na limeongezeka hadi kufikia
shilingi 1,660,532 mwaka 2013. “Nawapongeza wana Iringa kwa kuwa juhudi na
uchapakazi ambao umeufanya Mkoa kufikia hatua hiyo na kuwa wa pili baada ya Dar
es Salaam.” Alisema Mheshimiwa Pinda. Amesema kuwa pato hilo ni sawa na
shilingi 138,377 kwa mwezi au shilingi 4,612 kwa siku.
Amesema kuwa viashiria vya
kukua kwa uchumu ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa zenye umeme, elimu
bora, afya bora na vifaa vya mawasiliano. Amesema kulingana na taarifa ya
shirika la fedha Duniani, Tanzania imetoka miongoni mwa nchi 10 masikini Duniani
na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa.
Waziri Pinda ameutaka Mkoa wa
Iringa wenye fursa kubwa ya ardhi nzuri kwa kilimo cha mazao ya chakula na
biashara na hali ya hewa nzuri kutumia vizuri fursa hiyo. Amesema kuwa kuna
fursa nyingine za kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji katika ukanda wa chini.
Ameyasema hayo wakati Mkoa wa Iringa ukiwa na zaidi ya asilimia 80 ya wakazi
wanaotegemea kilimo. Mheshimiwa Pinda amesema kuwa uzalishaji wa mazao ni mzuri
na kuhakikisha kipo chakula cha nafaka ziada ya tani 1,032,613. Katika mwaka
ulioishia 2013/2014, mavuno yalifikia tani 1,379,602 za mazao ya chakula na
tani 77,622 za mazao ya biashara.
=30=
No comments:
Post a Comment