Na.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wasichana wenye umri wa miaka 14
mkoani Iringa wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma
za chanjo ili kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.
Rai hiyo ilitolewa na mkuu wa
mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akizindua chanjo mpya ya saratani ya
mlango wa kizazi mkoani Iringa iliyofanyika katika uwanja wa mashujaa mjini
Mafinga jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akikata utepe kuzindua utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mjini Mafinga |
Masenza alisema kuwa serikali
imeanzisha chanjo mpya ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri
wa miaka 14 nchini. Alisema kuwa chanjo hiyo ina lenga kuwakinga wasichana hao
dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.
“Serikali inawaomba wananchi
wetu wawahimize walengwa wote kufika katika kituo cha kutolea huduma za chanjo
na akina mama nao wajitokeze kwa wingi ili waweze kufanyiwa uchunguzi dhidi ya
ugonjwa wa saratani. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwakinga na magonjwa na
vifo, hii itaiwezesha serikali kutumia fedha ambazo zingetumika kugharamia
matibabu zitumike katika miradi mingine ya maendeleo” alisema Masenza.
Alisema kuwa, chanjo ni
uwekezaji katika uchumi wa taifa, serikali inatoa chanjo bila malipo katika
vituo vya serikali, binafsi na mashirika ya dini na yasiyo ya kiserikali.
Kwa kuwa chanjo ni uwekezaji
katika uchumi wa Taifa, serikali hutoa chanjo hizi bila malipo katika vituo
vyote vinavyotoa huduma za chanjo vikiwemo vya serikali, binafsi, mashirika ya
dini na yasiyo ya kiserikali.
=30=