Wednesday, April 25, 2018

WASICHANA MIAKA 14 KUCHANJWA DHIDI YA SARATANI YA KIZAZI IRINGA


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wasichana wenye umri wa miaka 14 mkoani Iringa wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za chanjo ili kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.

Rai hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akizindua chanjo mpya ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Iringa iliyofanyika katika uwanja wa mashujaa mjini Mafinga jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akikata utepe kuzindua utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mjini Mafinga

Masenza alisema kuwa serikali imeanzisha chanjo mpya ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 nchini. Alisema kuwa chanjo hiyo ina lenga kuwakinga wasichana hao dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Serikali inawaomba wananchi wetu wawahimize walengwa wote kufika katika kituo cha kutolea huduma za chanjo na akina mama nao wajitokeze kwa wingi ili waweze kufanyiwa uchunguzi dhidi ya ugonjwa wa saratani. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwakinga na magonjwa na vifo, hii itaiwezesha serikali kutumia fedha ambazo zingetumika kugharamia matibabu zitumike katika miradi mingine ya maendeleo” alisema Masenza.

Alisema kuwa, chanjo ni uwekezaji katika uchumi wa taifa, serikali inatoa chanjo bila malipo katika vituo vya serikali, binafsi na mashirika ya dini na yasiyo ya kiserikali.

Kwa kuwa chanjo ni uwekezaji katika uchumi wa Taifa, serikali hutoa chanjo hizi bila malipo katika vituo vyote vinavyotoa huduma za chanjo vikiwemo vya serikali, binafsi, mashirika ya dini na yasiyo ya kiserikali.
=30=

No comments:

Post a Comment