Thursday, March 15, 2012

WIKI YA MAJI IRINGA


Mkoa wa Iringa umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho  ya 24 ya wiki ya Maji kitaifa yatakayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 22 Machi, 2012.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) leo, amesema kuwa uzinduzi na kilele cha maadhimisho vitafanyika katika uwanja wa Samora uliopo katika Manispaa ya Iringa.
Amesema kuwa maadhimisho yaho yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘maji kwa usalama wa chakula’ yanalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu Sera ya Maji na majukumu ya wananchi katika kuitekeleza sera hiyo. Amesema madhumuni mengine ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji waprogramu ya maji, hali ya huduma ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na uhifadhi wa rasilimali za maji.
Dk. Christine amesema kuwa maadhimisho hayo pia yanalenga kutoa ujumbe kwa wadau kuhusu kaulimbiu ya wiki ya maji na siku ya maji Duniani na kuhamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki katika kupanga, ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji na usafi wa mazingira. Vilevile, maadhimisho ya wiki ya maji yanalenga kujenga na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wadau wa sekta hiyo.
Akiongelea maandalizi na matukio ya maadhimisho ya hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa maandalizi hayo yanaendelea vizuri na uzinduzi na kilele cha maadhimisho vitahusisha viongozi wa kitaifa. Amesema kuwa matukio ya mwaka 2012 yanalenga kuwashirikisha wadau na wananchi wote kwa pamoja kupanga, kujenga, kuendesha na kufanya matengeneza miradi ya maji na kuimarisha usafi wa mazingira sambamba na kutunza vyanzo vya maji.
Dk. Christine amezitaja shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo kuwa ni uzinduzi wa miradi ya maji ambayo ujenzi wake umekamilika. Amesema kuwa miradi mingi imetekelezwa kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji na wadau mbalimbali.
Kuhusu unufaishaji wa miradi hiyo itakayozinguliwa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa miradi hiyo itawanufaisha wananchi wapao 184,900.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa maadhimisho hayo kitaifa yatagharamiwa na Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mamlaka za Majisafi na majitaka nchini, Halmashauri, Taasisi na Mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali na wamiaji maji. Vilevile, amewashukuru wadau wote kwa utayari wao wa kuchangia ili kufanikisha maadhimisho hayo.
=30=


IRINGA MWENYEJI WIKI YA MAJI KITAIFA



Mkoa wa Iringa umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya 24 ya wiki ya Maji kitaifa ambapo shughuli na maonesho ya vifaa na teknolojia usambazaji maji na usafi wa mazingima vitafanyika ili kutoa ujumbe uliokusudiwa kwa wananchi.
 
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye ndiye mwenyeji wa maadhimisho hayo Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika katika Mkoa wa Iringa kuanzia tarehe 16-22 Machi, 2012. amesema “kilele cha maadhimisho kitakuwa tarehe 22 Machi ambayo  siku hiyo inafahamika Kimataifa kuwa ni Siku ya Maji Duniani kwa mujibu wa Azimio Na. 193/47 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa”. Amesema kuwa uzinduzi na kilele cha wiki ya maadhimisho hayo kitakuwa katika uwanja wa Samora, Manispaa ya Iringa.
 
Amesema miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika vyanzo vya maji, matanki na visima vya maji katika miji na vijiji mbalimbali mkoani Iringa.
 
Amesema kuwa shughuli nyingine ni maonesho ya vifaa na teknolojia za usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vitafanyika katika uwanja wa Samora uliopo katika Manispaa ya Iringa na kusisitiza kuwa maonesho yatafanyika muda wote wa maadhimishoyo ya wiki ya Maji.
 
Dk. Ishengoma amesema kuwa maadhimisho ya wiki ya maji mwaka 2012 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “maji na usalama wa chakula”. Kuhusu madhumuni ya maadhimisho hayo, amesema kuwa yanalenga kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa programu ya maji, hali ya huduma ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na uhifadhi wa rasilimali za maji. Maadhimisho hayo pia yanalenga kutoa ujumbe kwa wananchi juu ya kaulimbiu ya wiki ya maji na siku ya maji duniani pamoja na kuimarisha mshikamano baina ya wadau wa sekta ya maji.
 
Maadhimisho haya pia yanalenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika kupanga, ujenzi na uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji na usafi wa mazingira na kutoa elimu juu ya sera ya taifa ya maji na utekelezaji wake.
 
Kuhusu maandalizi ya wiki ya maji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa maandalizi yake yanaendelea vizuri na uzinduzi na kilele cha maadhimisho hayo vitawahususha viongozi wa kitaifa. Amesema kuwa shughuli mbalimbali zitafanyika katika maadhimisho hayo zikiwa ni uzinduzi wa miradi ya maji ambayo ujenzi wake umekamilika. Kuhusu ugharimiaji wa miradi hiyo, Dk. Ishengoma amesema kuwa miradi mingi imetekelezwa kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji na wadau mbalimbali. Amesema jumla ya wananchi 184,900 wananufaika na miradi itakayozinduliwa.
 
Ikumbukwe kuwa kila mwaka kuanzia mwaka 1988, Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Maji kuazia tarehe 16-22  Machi kwa kuwahusisha wananchi na wadau wote wa maji.