Thursday, March 15, 2012

WIKI YA MAJI IRINGA


Mkoa wa Iringa umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho  ya 24 ya wiki ya Maji kitaifa yatakayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 22 Machi, 2012.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) leo, amesema kuwa uzinduzi na kilele cha maadhimisho vitafanyika katika uwanja wa Samora uliopo katika Manispaa ya Iringa.
Amesema kuwa maadhimisho yaho yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘maji kwa usalama wa chakula’ yanalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu Sera ya Maji na majukumu ya wananchi katika kuitekeleza sera hiyo. Amesema madhumuni mengine ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji waprogramu ya maji, hali ya huduma ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na uhifadhi wa rasilimali za maji.
Dk. Christine amesema kuwa maadhimisho hayo pia yanalenga kutoa ujumbe kwa wadau kuhusu kaulimbiu ya wiki ya maji na siku ya maji Duniani na kuhamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki katika kupanga, ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji na usafi wa mazingira. Vilevile, maadhimisho ya wiki ya maji yanalenga kujenga na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wadau wa sekta hiyo.
Akiongelea maandalizi na matukio ya maadhimisho ya hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa maandalizi hayo yanaendelea vizuri na uzinduzi na kilele cha maadhimisho vitahusisha viongozi wa kitaifa. Amesema kuwa matukio ya mwaka 2012 yanalenga kuwashirikisha wadau na wananchi wote kwa pamoja kupanga, kujenga, kuendesha na kufanya matengeneza miradi ya maji na kuimarisha usafi wa mazingira sambamba na kutunza vyanzo vya maji.
Dk. Christine amezitaja shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo kuwa ni uzinduzi wa miradi ya maji ambayo ujenzi wake umekamilika. Amesema kuwa miradi mingi imetekelezwa kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji na wadau mbalimbali.
Kuhusu unufaishaji wa miradi hiyo itakayozinguliwa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa miradi hiyo itawanufaisha wananchi wapao 184,900.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa maadhimisho hayo kitaifa yatagharamiwa na Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mamlaka za Majisafi na majitaka nchini, Halmashauri, Taasisi na Mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali na wamiaji maji. Vilevile, amewashukuru wadau wote kwa utayari wao wa kuchangia ili kufanikisha maadhimisho hayo.
=30=


No comments:

Post a Comment