Thursday, November 2, 2017
MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA MKUU WA MKOA KATIKA KATA YA NDULI
MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA MKUU WA MKOA KATIKA KATA YA NDULI
MENEJA UWANJA WA NDEGE IRINGA APONGEZWA NA MKUU WA MKOA
Na Mwandishi Maalum, Iringa
Meneja
wa kiwanja cha ndege cha Iringa amepongezwa kwa kutatua matatizo ya jamii
inayouzunguka uwanja wa ndege wa Iringa.
Pongezi
hizo zilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mhe Amina Masenza alipokagua ujenzi
wa matundu 10 ya vyoo katika shule ya msingi Nduli iliyopo pembeni mwa uwanja
wa ndege wa Iringa katika kata ya Nduli.
Mhe
Masenza alisema “pongezi nyingi kwa
meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa. Tukiwa na watumishi wa umma 10 kama meneja
huyu, shule zote zingekuwa na vyoo bora na miundombinu madhubuti”.
Alisema kuwa
miundombinu bora inawafanya watoto kuipenda shule na walimu kuwahudumia vizuri
wanafunzi kwa kuwafundisha kwa moyo. Aliutaka uongozi wa shule hiyo kuvitunza
vizuri vyoo hivyo ili viweze kudumu na kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi.
Katika
taarifa ya mradi wa ujenzi wa choo matundu 10 ya wanafunzi iliyosomwa na mwl
Erick Kadope, alisema kuwa shule ya msingi Nduli ilikuwa na vyoo ambavyo si
rafiki kwa wanafunzi.
“Mheshimiwa mkuu wa
mkoa, kutokana na hali ya choo kuwa si rafiki kwa wanafunzi wetu, kiasi cha
kupelekea hofu ya kupatwa na magonjwa ya mlipuko, hivyo meneja wa uwanja wa
ndege wa Iringa, bi Hana Kibopile alichukulia uzito wa kipekee ili kunusuru
afya za watoto ili wafurahie masomo yao. Aliamua kutafuta mfadhili ambaye ni
mdau mkubwa wa maendeleo katika mkoa wa Iringa, anatoka kampuni ya Makota farm”
alisema mwl Kadope.
Akiongelea
ujenzi wa choo hicho, alisema kuwa ujenzi ulianza mwaka 2017 na umefikia 90%
ikiwa imebaki kazi ya kuweka mabomba ya ndani na kupaka rangi. Alisema kuwa
mradi huo umegharimu shilingi 28,000,000.
Ikumbukwe
kuwa Shule ya msingi Nduli ilianzishwa mwaka 1969.
=30=
BENDERA NYEKUNDU NYUMBA ZISIZO NA CHOO MANISPAA IRINGA
Na Mwandishi Maalum, Iringa
Mkuu
wa mkoa wa Iringa, mhe Amina Masenza ameiagiza halmashauri ya Manispaa ya Iringa
kuziwekea bendera nyekundu nyumba zote ambazo hazina vyoo bora na kuzipa muda
maalum wa kujenga na kukamilisha vyoo hivyo.
Agizo
hilo alilitoa katika shule ya msingi Nduli baada ya kupokea taarifa ya
utekelezaji wa ujenzi wa vyoo bora na usafi wa mazingira ya halmashauri ya Manispaa
ya Iringa kwa robo ya kwanza Julai-Septemba, 2017.
Mhe
Masenza alisema kuwa halmashauri ya Manispaa haina sababu ya kuwa na nyumba
isiyo na choo. “Sioni sababu ya
halmashauri ya Manispaa kuwa na nyumba ambayo haina choo bora, kwa sabababu
nyumba zote zinajengwa kwa ramani baada ya kutolewa kibali cha ujenzi kilichokubaliwa
na bwana afya baada ya kujiridhisha kuwa mchoro umebainisha ujenzi wa choo bora”
alisema mhe Masenza.
Aidha, aliitaka Manispaa ya Iringa kuziwekea bendera
nyekundu nyumba zote ambazo hazina vyoo bora na kuzipa muda maalum kukamilisha
ujenzi wa vyoo na kaya zitakazoshindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zichukuliwe.
Aliitaka Manispaa ya Iringa kuweka mkakati wa kukamilisha ujenzi wa vyoo kwa
kaya ambazo hazina vyoo.
Wakati
huohuo, mkuu wa mkoa alimtaka mkuu wa wilaya ya Iringa kutoa maelezo ya sababu
zinazofanya baadhi ya nyumba katika Manispaa ya Iringa kutokuwa na vyoo.
Mkuu
wa mkoa wa Iringa, alifanya ziara ya siku moja katika kata ya Nduli, Manispa ya
Iringa kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo.
=30=
NGOs ZATAKIWA KUFANYA KAZI ZINAZOONEKANA
Na Mwandishi Maalum, Iringa
Mashirika
yasiyo ya kiserikali yanayotaka kufanya kazi kuwahudumia wananchi mkoani Iringa
yatakiwa kufanya kazi zinazoonekana na kupimika.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza alipokuwa akiongea
na jumuiya ya shule ya msingi Nduli iliyopo katika Manispaa ya Iringa
alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi
wa vyoo katika kata ya Nduli.
Mhe
Masenza alisema kuwa mashirika yote yasiyo ya kiserikali yanayotaka kufanya
kazi za kuwahudumia wananchi mkoani Iringa, lazima yaeleze kazi zitakazofanyika
na ziwe zinazoonekana na kupimika.
Alisema kuwa yapo mashirika yasiyo ya
kiserikali ambayo yamekuwa yakipata fedha kwa kusingizio cha kuwahudumia
wananchi katika usafi wa mazingira lakini yamekuwa hayafanyi hivyo. Alisema kuwa
anataka mashirika makini na yanayowajibika kwa wananchi na serikali katika
utekelezaji wa majukumu yake.
Akiongelea
hali ya usafi wa mazingira katika kata ya Nduli, mkuu wa mkoa alisema kuwa hali
ya usafi wa mazingira hairidhishi.
“Katika ziara hii tumejionea jinsi maeneo
mengi yalivyotapakaa takataka, nichukue nafasi hii kuwaagiza watendaji wote,
kusimamia ipasavyo zoezi la usafi katika maeneo wanayoyasimamia. Haipendezi kusimamiwa
na viongozi katika kazi ambazo ni majukumu yenu ya kila siku” alisema mhe Masenza.
=30=
Subscribe to:
Posts (Atom)