Thursday, November 2, 2017

MENEJA UWANJA WA NDEGE IRINGA APONGEZWA NA MKUU WA MKOA



Na Mwandishi Maalum, Iringa

Meneja wa kiwanja cha ndege cha Iringa amepongezwa kwa kutatua matatizo ya jamii inayouzunguka uwanja wa ndege wa Iringa.

Pongezi hizo zilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mhe Amina Masenza alipokagua ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika shule ya msingi Nduli iliyopo pembeni mwa uwanja wa ndege wa Iringa katika kata ya Nduli.

Mhe Masenza alisema “pongezi nyingi kwa meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa. Tukiwa na watumishi wa umma 10 kama meneja huyu, shule zote zingekuwa na vyoo bora na miundombinu madhubuti”

Alisema kuwa miundombinu bora inawafanya watoto kuipenda shule na walimu kuwahudumia vizuri wanafunzi kwa kuwafundisha kwa moyo. Aliutaka uongozi wa shule hiyo kuvitunza vizuri vyoo hivyo ili viweze kudumu na kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi.

Katika taarifa ya mradi wa ujenzi wa choo matundu 10 ya wanafunzi iliyosomwa na mwl Erick Kadope, alisema kuwa shule ya msingi Nduli ilikuwa na vyoo ambavyo si rafiki kwa wanafunzi. 

Mheshimiwa mkuu wa mkoa, kutokana na hali ya choo kuwa si rafiki kwa wanafunzi wetu, kiasi cha kupelekea hofu ya kupatwa na magonjwa ya mlipuko, hivyo meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa, bi Hana Kibopile alichukulia uzito wa kipekee ili kunusuru afya za watoto ili wafurahie masomo yao. Aliamua kutafuta mfadhili ambaye ni mdau mkubwa wa maendeleo katika mkoa wa Iringa, anatoka kampuni ya Makota farm” alisema mwl Kadope.    

Akiongelea ujenzi wa choo hicho, alisema kuwa ujenzi ulianza mwaka 2017 na umefikia 90% ikiwa imebaki kazi ya kuweka mabomba ya ndani na kupaka rangi. Alisema kuwa mradi huo umegharimu shilingi 28,000,000.

Ikumbukwe kuwa Shule ya msingi Nduli ilianzishwa mwaka 1969.
=30=


No comments:

Post a Comment