Thursday, November 2, 2017

BENDERA NYEKUNDU NYUMBA ZISIZO NA CHOO MANISPAA IRINGA



Na Mwandishi Maalum, Iringa

Mkuu wa mkoa wa Iringa, mhe Amina Masenza ameiagiza halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuziwekea bendera nyekundu nyumba zote ambazo hazina vyoo bora na kuzipa muda maalum wa kujenga na kukamilisha vyoo hivyo.

Agizo hilo alilitoa katika shule ya msingi Nduli baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa vyoo bora na usafi wa mazingira ya halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa robo ya kwanza Julai-Septemba, 2017.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza

Mhe Masenza alisema kuwa halmashauri ya Manispaa haina sababu ya kuwa na nyumba isiyo na choo. “Sioni sababu ya halmashauri ya Manispaa kuwa na nyumba ambayo haina choo bora, kwa sabababu nyumba zote zinajengwa kwa ramani baada ya kutolewa kibali cha ujenzi kilichokubaliwa na bwana afya baada ya kujiridhisha kuwa mchoro umebainisha ujenzi wa choo bora” alisema mhe Masenza. 

Aidha, aliitaka Manispaa ya Iringa kuziwekea bendera nyekundu nyumba zote ambazo hazina vyoo bora na kuzipa muda maalum kukamilisha ujenzi wa vyoo na kaya zitakazoshindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zichukuliwe. Aliitaka Manispaa ya Iringa kuweka mkakati wa kukamilisha ujenzi wa vyoo kwa kaya ambazo hazina vyoo.

Wakati huohuo, mkuu wa mkoa alimtaka mkuu wa wilaya ya Iringa kutoa maelezo ya sababu zinazofanya baadhi ya nyumba katika Manispaa ya Iringa kutokuwa na vyoo.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, alifanya ziara ya siku moja katika kata ya Nduli, Manispa ya Iringa kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo.
=30=

No comments:

Post a Comment