Thursday, November 2, 2017

NGOs ZATAKIWA KUFANYA KAZI ZINAZOONEKANA



Na Mwandishi Maalum, Iringa
Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotaka kufanya kazi kuwahudumia wananchi mkoani Iringa yatakiwa kufanya kazi zinazoonekana na kupimika.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza alipokuwa akiongea na jumuiya ya shule ya msingi Nduli iliyopo katika Manispaa ya Iringa alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo katika kata ya Nduli.

Mhe Masenza alisema kuwa mashirika yote yasiyo ya kiserikali yanayotaka kufanya kazi za kuwahudumia wananchi mkoani Iringa, lazima yaeleze kazi zitakazofanyika na ziwe zinazoonekana na kupimika. 

Alisema kuwa yapo mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakipata fedha kwa kusingizio cha kuwahudumia wananchi katika usafi wa mazingira lakini yamekuwa hayafanyi hivyo. Alisema kuwa anataka mashirika makini na yanayowajibika kwa wananchi na serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akiongelea hali ya usafi wa mazingira katika kata ya Nduli, mkuu wa mkoa alisema kuwa hali ya usafi wa mazingira hairidhishi. 

“Katika ziara hii tumejionea jinsi maeneo mengi yalivyotapakaa takataka, nichukue nafasi hii kuwaagiza watendaji wote, kusimamia ipasavyo zoezi la usafi katika maeneo wanayoyasimamia. Haipendezi kusimamiwa na viongozi katika kazi ambazo ni majukumu yenu ya kila siku” alisema mhe Masenza.
=30=

No comments:

Post a Comment