Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Jamii
imetakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na kikundi cha kudhibiti kifua kikuu
mkoa wa Iringa (KIKUKI) ili kiweze kuwaibua wahisiwa wa ugonjwa wa kifua kikuu
mkoani hapa.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu wa KIKUKI, Lucas Mallya alipokuwa akiongelea
changamoto zinazokikabili kikundi chao kutekeleza majukumu yake katika kampeni
tambuzi za kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza katika bustani ya Manispaa ya
Iringa hivi karibuni.
Mallya
alisema “changamoto kubwa katika kikundi
chetu ni watu na wadau wa kutuunga mkono katika kazi tunazofanya za kuibua
wahisiwa wa ugonjwa wa kifua kikuu, kuwapeleka kufanyiwa uchunguzi na
kuanzishiwa dawa”.
Alisema kuwa kikundi kinahitaji posho na nauli kwa ili wanakikundi
waweze kutembelea maeneo tofauti katika kata 18 za Manispaa ya Iringa. Alisema
kuwa Kata 18 ni nyingi na kubwa hivyo kuzifikia zote ni kazi inayohitaji moyo
wa kujitoa na malipo kidogo.
Changamoto
nyingine aliitaja kuwa ni imani potofu waliyonayo wananchi kuwa ugonjwa wa
kifua kikuu unatokana na kurogwa, hivyo matibabu yake kufanyika kwa waganga wa
kienyeji.
“Ugonjwa wa kifua kikuu
unatibika hospitali tena bure. Katika kuthibitisha hili, kikundi chetu kipo hapa
kutoa ushuhuda kwa sababu wanakikundi ni watu waliougua ugonjwa wa kifua kikuu
na kupona” alisema Mallya.
Nae mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Iringa, Dr. Tecla Orio alisema kuwa kikundi cha KIKUKI kimekuwa kikifanya kazi nzuri kwa kujitolea katika Manispaa ya Iringa. Alitoa wito kwa wadau wa mapambano dhidi ya Kifua Kikuu kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo ili kikundi kiweze kuwafikia na kuwaibua wagonjwa wengi zaidi na kuanzishiwa tiba.
Kikundi
cha kudhibiti kifua kikuu mkoa wa Iringa, kilianza mwaka 2011 kikiwa na
wanakikundi 23. Kikundi kinatumia njia za ngoma, maigizo na kutoa ushuhuda
katika kufikia ujumbe kwa wahusika.
=30=