Na. Revocatus Kassimba, Songea
Serikali mkoani Ruvuma imeihakikishia nchi ya Cuba kuendeleza ushirikiano ili kuboresha mahusiano mema yaliyojengeka kwa miongo zaidi ya minne hususan katika kuendeleza huduma za afya nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Songea na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Dkt Anselm Tarimo alipokuwa akiongea na Balozi wa Cuba nchini Ernesto Gomez Diaz alipofanya mazungumzo na uongozi wa Sekretariati ya Mkoa wa Ruvuma.
Dkt Tarimo alielezea Uhusiano wa kiurafiki uliopo na nchi ya Cuba kuwa umesaidia sana katika jitihada za serikali ya Tanzania kuwapatia wananchi wake Huduma bora na za uhakika za afya.
Alisema kwa kipindi kirefu nchi ya Cuba imekuwa ikisaidia Tanzania kwa kuipatia wataalam wa afya hususan madaktari wanaofanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini ambapo katika mkoa wa Ruvuma wapo madaktari wawili kutoka nchini Cuba.
“Tunashukuru kwa ushirikiano tulionao baina ya nchiz zetu mbili kwani kuanzia miaka ya 1980 mkoa wetu umekuwa ukipokea madaktari kutoka nchini Cuba ambao wanasaidia kutoa Huduma za tiba katika hospitali yetu ya Mkoa Songea” alisema Dkt Tarimo
Aliongeza kusema kwa sasa mahitaji ya madaktari ni makubwa kutokana na hospitali ya mkoa kupandishwa hadhi na kuwa ya rufaa hivyo ni vema Cuba ikaongeza wataalam zaidi
Naye Balozi wa Cuba nchini Ernesto Gomez Diaz alishukuru serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kwa kuendeleza na kudumisha ushirikiano kati ya nchi zote mbili toka enzi za waasisi Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Fidel Castro wa Cuba
Balozi Diaz amesema Cuba ni nchi pekee iliyobaki inayofuata mfumo wa Ukoministi Duniani wenye lengo la kuhakikisha maisha ya kijamaa ambapo rasilimali za umma zinatumika kwa wote
Aliongeza kusema kuwa katika nchi ya Cuba kutokana na sera ya Ukoministi serikali imefanikiwa kutoa Huduma za afya na Elimu bure kwa raia wake wote na kusema kuwa nchi yake itaendelea kutoa kipaumbele kwa watanzania kwenda kusoma udaktari nchini Cuba .
Balozi Diaz yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo amepata fursa ya kutembelea na kukagua Hospitali ya mkoa ambapo nchi yake ina madaktari wawili wanaofanya kazi.
Ameshukuru uongozi wa serikali kwa kutoa ushirikiano kwa wataalam hao wa Cuba kwa kipindi chote wanachofanya kazi kwani wameendelea kufurahi uwepo wao hapa mkoani.