Tuesday, May 22, 2018

IRINGA WATAKIWA KUJITOKEZA KUPOKEA UJUMBE WA MWENGE WA UHURU


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wananchi mkoani Iringa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru utakaoanza mbio zake mkoani hapa kesho.

Wito huo ulitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu ujio wa Mwenge wa Uhuru mkoani Iringa hapo kesho.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa Mwenge Uhuru utaingia mkoani Iringa kesho tarehe 23/5/2018 ukitokea mkoani Mbeya na utakimbizwa katika halmashauri tano za mkoa wa Iringa. Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Iringa, Kilolo, Manispaa ya Mji Mafinga kabla ya kukabidhiwa mkoani Njombe tarehe 28/5/2018. 

Napenda kutoa wito kwa wananchi kwenye Halmashauri zote kujitokeza kwa wingi kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru. Aidha, wananchi wote bila kujali itikadi zao kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru ikiwa ni pamoja na kwenye viwanja vya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru, miradi ya maendeleo, maeneo ya kutolea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru na kwenye viwanja vya mikesha” alisema Masenza.

Aidha, alivitaka vyombo vya habari, kushiriki kikamilifu katika kuufikisha ujumbe wa Mwenge wa Uhuru kwa wananchi na kuwahamasisha kufika kwenye maeneo ambako ujumbe utatolewa.
=30=

No comments:

Post a Comment