Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma amesema kuwa elimu kwa umma ni nyenzo muhimu sana katika
kuwaandaa wananchi kuhama kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analojia na
kuingia katika mfumo wa digitali.
Ameyasema hayo katika mkutano wa
viongozi wa mkoa wa Iringa kuhusiana na mabadiliko ya mfumo wa utangazaji
kutoka analojia kwenda digitali uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo
kikuu Huria, tawi la Iringa.
Amesema katika kufanikisha jitihada
hizo, “umeonekana umuhimu wa kuelimisha umma kwa kushirikisha wizara, idara za
Serikali pamoja na wananchi wote ili kuweza kufanikisha mabadiliko haya kwa
ufanisi bila kuathiri upatikanaji wa huduma za utangazaji nchini”. Ameishauri
kamati maalumu ya kitaifa inayofanya kazi ya kuwaelimisha wananchi nchini juu
ya mabadiliko ya teknolojia ya utangazaji kuhakikisha wananchi wengi wanapata
elimu hiyo ili kuwaandaa na mabadiliko hayo. Amesema maana ya mabadiliko ya
teknolojia, matarajio ya baada ya mabadiliko na wajibu wa mwananchi katika
kufanikisha mabadiliko hayo ni mambo ya muhimu kutiliwa mkazo katika utoaji wa
elimu kwa wananchi.
Akiongelea Sensa ya Watu na Makazi,
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ametoa wito kwa washiriki hao kuuelimisha umma juu ya
umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi. Amesema “natoa wito kwenu washiriki wa
mkutano huu hasa waandishi wa habari kutumia nafasi hii kuhimiza jambo hili na
kutumia muda wenu na vyombo vyenu kuwaelimisha wananchi ili waweze kushiriki
katika zoezi hili na kulifanya liwe la manufaa na kuleta tija katika Mkoa wetu
wa Iringa na Taifa kwa ujumla” alisisitiza Dkt Christine.
=30=