Wazazi wameshauriwa kutoa
ushirikiano kwa walimu katika malezi ya wanafunzi ili kuhakikisha jamii inakuwa
na watu wenye nidhamu na maadili mema.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alikokuwa akiongea na wananchi, walimu na
wanafunzi wa shule ya sekondari Ilambilole iliyopo katika Kata ya Nduli,
Wilayani Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa suala la
nidhamu kwa wanafunzi haliishii shuleni pekee bali ni jukumu la jamii nzima
kuhakikisha inawasaidia walimu katika malezi ya wanafunzi. Amesema “nidhamu
inaanzia nyumbani hivyo lazima tusaidiane na walimu katika kudumisha nidhamu ya
watoto wetu, lakini tukiwaachia walimu peke yao hatuwezi kufanikiwa. Walimu
wana nafasi yao katika kukuza na kudumisha nidhamu na wazazi pia wana nafasi
yao katika hili”.
Akiongelea changamoto ya upungufu wa
walimu wanaofundisha masomo ya sayansi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa
upungufu huo upo kwa sababu wanafunzi wengi hawataki kusoma masomo ya sayansi.
“Tunaupungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwa sababu watoto wetu hawasomi
masomo ya sayansi” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Katika kukabiliana na
hali hiyo, alishauri wanafunzi wahamasishwe kusoma masomo ya sayansi ili kuweza
kuziba pengo hilo. Aidha, alisema kuwa Serikali inaendelea na mipango ya muda
mrefu ya kuhakikisha changamoto hiyo inabaki historia.
Akiwasilisha taarifa ya shule ya
Sekondari ya Ilambilole, Mkuu wa shule hiyo, Vicent Ngaya amesema kuwa shule
yake inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba za walimu na walimu wa
masomo ya sayansi. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni kukosekana kwa mabweni
hasa kwa wanafunzi wa kike na umbali wa makazi ya walimu kutoka shuleni jambo
linalosababisha kuchelewa kufika shuleni na kufika wakiwa wamechoka sana.
Kuhusu ufauli, Ngaya amesema kuwa
shule imepata mafanikio makubwa katika ufaulu wa wanafunzi, ambapo kwa mwaka
2010 ufaulu ulikuwa ni asilimia 78 na mwaka 2011 ufaulu ulikuwa ni asilimia 61.
Wakati huohuo, suala la wivu
limeelezwa kuwa halina nafasi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi
litakalofanyika usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti, mwaka huu. Kauli hiyo
imetolewa na Mratibu Msaidizi wa Sensa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga wakati
akifafanua masuala mbalimbali ya Sensa katika Kijiji cha Ikengeza, Wilaya ya
Iringa. Millinga amewataka akina baba kutokuwa na dhana ya wivu wa aina yoyote
pindi wake zao watakapokuwa wakihojiwa na makarani wa Sensa kwa sababu baadhi
ya maswali yatawahusu akina mama pekee. Amesema maswali hayo hayatahusiana na
ndoa bali ni masuala ya uzazi na kuwataka kuwapatia uhuru na nafasi pindi
watakapokuwa wanahojiwa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi.
Millinga amesema kuwa Sensa ya Watu
na Makazi ni muhimu sana kwa nchi kwa sababu pasipo kufahamu idadi sahihi ya
watu inawezekana wananchi kupewa huduma pungufu ya mahitaj yao. Amesema Sensa
hiyo itawahusisha watanzania wote na wageni watakaokuwa ndani ya nchi siku hiyo
ya Sensa.
=30=
No comments:
Post a Comment