Thursday, April 12, 2012

MALEZI YA WATOTO YAHIMIZWA IRINGA

Na. Dennis Gondwe, IRINGA
Serikali Mkoani Iringa imesema kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi binafsi katika kuhakikisha kuwa malezi mazuri yanatolewa kwa watoto na kuwasaidia watoto walio katika mazingira hatarishi ili nao waweze kufurahia matunda ya uhuru kama watoto wengine kwa kuwa na maadili mema.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa na Mwl. Joseph Mnyikambi, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Huduma za Jamii iliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa katika hafla ya ugawaji wa zawadi kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wa Manispaa ya Iringa chini ya shirika lisilo la kiserikali la Operation Christmas Child lenye makao yake Makuu nchini Marekani iliyofanyika katika ukumbi wa IDYDC Manispaa ya Iringa.

Mwl. Mnyikambi amesema kuwa “nimefahamishwa kuwa taasisi hii ya OCC pia inatoa mafunzo yanayolenga maadili. Nawapongeza sana kwa sababu jamii yenye maadili mema ndiyo jamii inayofanikiwa katika maisha”.

Amesema kuwa “ili jamii ifanikiwe katika maisha basi msingi wake lazima jamii hiyo iwekeze katika malezi na makuzi ya watoto katika maadili”. Ametoa wito kwa jamii kulipa kipaumbele suala la maadili kwa watoto na vijana ili kujenga taifa imara na makini.

Amesema kuwa suala la maadili ni suala la upendo katika jamii na kusisitiza kuwa kinyume chake ni mmomonyoko wa maadili katika taifa zima. Amesema kuwa jamii kwa sasa inashuhudia watoto wakitumia dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, lugha za matusi na watoto wa kiume kusuka nywele jambo linalowafananisha na watoto wa kike na kufanya vitendo visivyo vya kibinadamu kama ubakaji wa watoto wadogo.

Katika risala yao iliyosomwa na Mratibu wa Operation Christmas Child Askofu Dk. Boaz Sollo ameishukuru serikali kwa kusamehe kodi na kuiomba kupitia mamlaka ya bandari kuweka mfumo rahisi zaidi wa kutoa vitu bandarini ili kupunguza au kuondoa gharama zinazotokana na uhifadhi wa mizigo hiyo bandarini.

Aidha, ameishauri serikali kuwa macho zaidi na yeyote anayejaribu kuhatarisha amani kwa kutumia dini au siasa ili nchi iiendelee kuwa na amani na utulivu. Amesema kuwa mwaka huu kwa Mkoa wa Iringa umepokea jumla ya mabox 3500 ya zawadi kwa ajili ya watoto 3500.

=30=