Tuesday, February 20, 2018
SERIKALI YATOA MASHARTI MATATU KUFUNGULIWA NGODI WA NYAKAVANGALA
Na. Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa
Serikali yatoa
masharti matatu kufungua mgodi wa kuzalisha dhahabu Nyakavangala na kuelekeza
yatekelezwe ndani ya wiki mbili.
Masharti hayo
ambayo ni kupitisha kanuni za uchimbaji madini, wataalam kutoka wizara ya
madini kukagua mashimo yote ya kuchimba dhahabu na mafunzo ya usalama katika
machimbo yalitolewa na naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko aliyefanya ziara ya
siku moja katika mgodi wa Nyakavangala uliopo katika Kata ya Malengamakali
wilayani Iringa jana.
Biteko alisema kabla
ya kufunguliwa mgodi huo mambo hayo matatu lazima yafanyiwe kazi ili kufanya
mazingira ya uchimbaji dhahabu kuwa salama. Katika kuhakikisha mazingira
yanakuwa sawa, aliwataka wachimbaji hao kuwa wakweli na wazalengo kwa nchi yao
katika kiasi cha dhahabu kinachozalishwa mgodini hapo. Akiongelea utoroshaji
madini hayo, alisema “mchimbaji
anayedhani serikali ya Dr. John Magufuli anaweza kutorosha dhahabu atafute kazi
nyingine” alisema Biteko.
Aliongeza kuwa serikali ipo makini kuhakikisha
madini hayo yanawanufaisha watanzania na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Awali mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa katika kuhakikisha hali ya machimbo dhahabu
ya Nyakavangala inakuwa salama, kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Iringa
iliagiza ufanyike ukaguzi katika mashimo yote yanayochimba dhahabu katika mgodi
huo. Alisema lengo la ukaguzi huo ni kuwahakikishia usalama wachimbaji hao na
kuepuka vifo vitokanavyo na mashimo hayo kuanguka.
=30=
MASENZA AWATAKA WAFANYA BIASHARA KULIPA KODI
Na Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imewataka
wafanyabiashara wote kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ili serikali iweze
kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisalimia wachimbaji wadogo wa mgodi wa
nyakavangala katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyakavangala
kilichopo wilayani Iringa alipokuwa akiongea na wachimbaji wadogo wakati wa
ziara ya naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko mkoani Iringa jana.
Masenza alisema “katika Mkoa wangu, siruhusu mtu yeyote
kufanya biashara bila kulipa kodi. Lazima kulipa kodi. Kodi ndiyo inajenga
zahanati, kodi ndiyo inajenga shule na miundombinu yote na kodi ndiyo inalipa
mishahara”.
Alisema kuwa utamaduni wa kulipa kodi ndiyo utawezesha ujenzi
wa barabara ya kuelekea katika machimbo ya Nyakavangala kwa kiwango
kinachoridhisha.
Aidha, pamoja na kuwapa pole wachimbaji
wa dhahabu wa Nyakavangala kufuatia vifo vilivyotokana na ajali zilizotokea
siku za nyuma katika mgodi huo, aliwataka kuzingatia kanuni za usalama. “Sitaki
vifo katika Mkoa wangu. Lazima kanuni za usalama zizingatiwe wakati wa
uchimbaji wa dhahabu”.
Alisema kuwa ushauri wa wakaguzi wa madini uzingatiwe
ili machimbo ya Nyakavangala yawe eneo salama kwa wachimbaji wadogo mkoani Iringa.
Wakati huohuo, mkuu wa Mkoa wa
Iringa alimuagiza mkuu wa Wilaya hiyo kwenda kuwasikiliza wananchi waliojaribu
kubeba mabango katika ziara ya naibu waziri wa Madini ili kufahamu hoja zao na
kuzitafutia ufumbuzi.
Akiongea katika majumuisho ya
ziara yake yaliyofanyika katika ofisi ya mkuu wa Mkoa, naibu waziri wa Madini,
Dotto Biteko alisema kuwa nchi imempata kiongozi anayethubutu kuhakikisha
madini yanawanufaisha watanzania.
“Rais, Dr
John Magufuli ana dhamira ya dhati kuyafanya madini yawanufaishe wananchi wa
Tanzania na kuchangia katika pato la taifa. Dhamira yake ni kuona madini
yanawanufaisha wachimbaji wadogo na hatimae kufikia hatua ya uchimbaji mkubwa”
alisema Biteko.
=30=
WACHIMBAJI NYAKAVANGALA WATAKIWA KUJIHADHARI NA UKIMWI
Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Serikali mkoani
Iringa imewataka wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Nyakavangala
wilayani Iringa kujihadhari ya maambukizi ya virus vya Ukimwi mgodini hapo.
Kauli hiyo
ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akihutubia mkutano
wa hadhara wa wachimbaji wadogo katika kijiji cha Nyakavanga wilayani Iringa
leo.
Masenza alisema
kuwa maambukizi ya virus vya Ukimwi katika Mkoa wa Iringa yapo kwa kiwango cha
juu. Aliwataka wachimbaji wadogo katika mgodi wa Nyakavangala kujitunza ili
kutokupata maambukizi hayo. Alisema asilimia kubwa ya wachimbaji ni vijana
ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.
Iwapo nguvu kazi hiyo itaugua ugonjwa wa Ukimwi
familia zao zitapoteza nguvu kazi na Taifa pia. Vilevile, aliwakumbusha kuwa
kipindupindu bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo yenye mikusanyiko ya
watu wengi.
=30=
Subscribe to:
Posts (Atom)