Na. Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa
Serikali yatoa
masharti matatu kufungua mgodi wa kuzalisha dhahabu Nyakavangala na kuelekeza
yatekelezwe ndani ya wiki mbili.
Masharti hayo
ambayo ni kupitisha kanuni za uchimbaji madini, wataalam kutoka wizara ya
madini kukagua mashimo yote ya kuchimba dhahabu na mafunzo ya usalama katika
machimbo yalitolewa na naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko aliyefanya ziara ya
siku moja katika mgodi wa Nyakavangala uliopo katika Kata ya Malengamakali
wilayani Iringa jana.
Biteko alisema kabla
ya kufunguliwa mgodi huo mambo hayo matatu lazima yafanyiwe kazi ili kufanya
mazingira ya uchimbaji dhahabu kuwa salama. Katika kuhakikisha mazingira
yanakuwa sawa, aliwataka wachimbaji hao kuwa wakweli na wazalengo kwa nchi yao
katika kiasi cha dhahabu kinachozalishwa mgodini hapo. Akiongelea utoroshaji
madini hayo, alisema “mchimbaji
anayedhani serikali ya Dr. John Magufuli anaweza kutorosha dhahabu atafute kazi
nyingine” alisema Biteko.
Aliongeza kuwa serikali ipo makini kuhakikisha
madini hayo yanawanufaisha watanzania na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Awali mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa katika kuhakikisha hali ya machimbo dhahabu
ya Nyakavangala inakuwa salama, kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Iringa
iliagiza ufanyike ukaguzi katika mashimo yote yanayochimba dhahabu katika mgodi
huo. Alisema lengo la ukaguzi huo ni kuwahakikishia usalama wachimbaji hao na
kuepuka vifo vitokanavyo na mashimo hayo kuanguka.
=30=
No comments:
Post a Comment