Na Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imewataka
wafanyabiashara wote kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ili serikali iweze
kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisalimia wachimbaji wadogo wa mgodi wa
nyakavangala katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyakavangala
kilichopo wilayani Iringa alipokuwa akiongea na wachimbaji wadogo wakati wa
ziara ya naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko mkoani Iringa jana.
Masenza alisema “katika Mkoa wangu, siruhusu mtu yeyote
kufanya biashara bila kulipa kodi. Lazima kulipa kodi. Kodi ndiyo inajenga
zahanati, kodi ndiyo inajenga shule na miundombinu yote na kodi ndiyo inalipa
mishahara”.
Alisema kuwa utamaduni wa kulipa kodi ndiyo utawezesha ujenzi
wa barabara ya kuelekea katika machimbo ya Nyakavangala kwa kiwango
kinachoridhisha.
Aidha, pamoja na kuwapa pole wachimbaji
wa dhahabu wa Nyakavangala kufuatia vifo vilivyotokana na ajali zilizotokea
siku za nyuma katika mgodi huo, aliwataka kuzingatia kanuni za usalama. “Sitaki
vifo katika Mkoa wangu. Lazima kanuni za usalama zizingatiwe wakati wa
uchimbaji wa dhahabu”.
Alisema kuwa ushauri wa wakaguzi wa madini uzingatiwe
ili machimbo ya Nyakavangala yawe eneo salama kwa wachimbaji wadogo mkoani Iringa.
Wakati huohuo, mkuu wa Mkoa wa
Iringa alimuagiza mkuu wa Wilaya hiyo kwenda kuwasikiliza wananchi waliojaribu
kubeba mabango katika ziara ya naibu waziri wa Madini ili kufahamu hoja zao na
kuzitafutia ufumbuzi.
Akiongea katika majumuisho ya
ziara yake yaliyofanyika katika ofisi ya mkuu wa Mkoa, naibu waziri wa Madini,
Dotto Biteko alisema kuwa nchi imempata kiongozi anayethubutu kuhakikisha
madini yanawanufaisha watanzania.
“Rais, Dr
John Magufuli ana dhamira ya dhati kuyafanya madini yawanufaishe wananchi wa
Tanzania na kuchangia katika pato la taifa. Dhamira yake ni kuona madini
yanawanufaisha wachimbaji wadogo na hatimae kufikia hatua ya uchimbaji mkubwa”
alisema Biteko.
=30=
No comments:
Post a Comment